Huku Chama kule Tuisila tutaelewana tu!

Muktasari:
Nyota wanaotajwa zaidi kuleta ushindani kwa timu hizo ni Clatous Chama, Joash Onyango na Larry Bwalya (Simba), Mukoko Tonombe na Tuisila Kisinda (Yanga).
KATIKA mtihani mkubwa walionao mastaa wa Simba na na Yanga ni kuendeleza makali yao mbele ya mashabiki. Nyota watano wa Simba na Yanga, wanatajwa kuwa tishio katika ushindani wa Ligi Kuu Tanzania Bara inayoanza kutimua vumbi Jumapili ijayo.
Nyota wanaotajwa zaidi kuleta ushindani kwa timu hizo ni Clatous Chama, Joash Onyango na Larry Bwalya (Simba), Mukoko Tonombe na Tuisila Kisinda (Yanga).
Akizungumzia usajili wa vikosi vya Yanga Simba, Azam na Namungo, aliyewahi kuwa kocha wa Simba Jamhuri Kihwelo Julio alisema wachezaji kama Mukoko na Kisinda wataleta ushindani zaidi katika ligi, kwani licha ya kuwaona katika mchezo mmoja aligundua wana vitu katika miguu yao.
“Yanga wanahitaji sana muunganiko, maana hata benchi la ufundi wote ni wageni lakini kwa usajili walioufanya utasaidia kuleta ushindani katika Ligi yetu, ila wanahitaji sana muda wa kukaa pamoja ili kutengeneza muunganiko ambao Simba waliutengeneza muda mrefu,”a lisema Julio
“Hata uwakilishi wa kimataifa kwa upande wa Simba sina wasiwasi sana, kutokana na wachezaji waliowaongeza katika dirisha la usajili, wanauzoefu wa michuano ya kimataifa hivyo watawasaidia, lakini kikosi cha Namungo nimekitazama naona watapata tabu katika ushiriki wao,” alisema.
Hitimana Thiery ambaye ni Kocha wa Namungo alisema timu nyingi zimefanya usajili mzuri na wenye mantiki kwa timu zao tofauti na timu yake ambayo inabidi kutumia muda mwingi kujiweka sawa.
Katika wachezaji ambao Namungo imesajili ni nyota wawili pekee Humoud aliyetokea Mtibwa Sugar na Shiza Kichuya wa Simba ndio walikuwa mapendekezo yake wengine ni wa jopo la viongozi.
Hitimana alisema, Simba inawachezaji wenye uwezo binafsi kuanzia mchezaji mwenyewe mpaka timu nzima, huku kwa upande wa Yanga alisema hajawaona vizuri.
Alisema atapambana na kikosi hicho hicho alichokuwa nacho katika Ligi na pia michuano ya kimataifa na ana imani watapiga hatua.
“Tutautumia muda huu wa takribani mwezi na nusu kujiandaa zaidi na Kombe la Shirikisho kupitia mechi za Ligi Kuu ambazo zitatufanya tuzidi kuwa bora zaidi, katika hilo hakuna shida kabisa,” alisema.
Naye Kocha Fredy Felix ‘Minziro’ alisema; “Simba ina timu bora sana siwezi kuizungumzia kwa kuwa iko vizuri na hata Yanga nao wamejitahidi kufanya usajili, sema cha msingi wanatakiwa kuwaacha benchi la ufundi lifanye majukumu yake na uongozi ufanye yake.
“Simba ni timu bora hata usajili wao wameongeza watu wazuri kwa mahitaji yao ya kimataifa, sina shaka kabisa na wao, hata Azam pia wamejitahidi kadri ya uwezo wao hivyo ushindani utakuwa mkali sana maana mbali na hao wa kimataifa lakini ubingwa wa Ligi Kuu utakuwa na ushindani,” aliongeza mchezaji huyo wa zamani wa Yanga na Taifa Stars.
Mkuu wa Idara ya habari ya Azam FC, Thabit Zakaria ‘Zaka Zakazi’, alisema; “Msimu huu tunahitaji kombe kubwa moja kati ya hayo makubwa, ambalo ni la Ligi Kuu basi likishindikana hata la FA ni kubwa pia huu ndio mpango wetu msimu tunaouanza.”
KANDA YA ZIWA
Mashabiki wa Simba na Yanga jijini Mwanza wameanza tambo kwa kila upande ukijinasibu usajili wa baadhi ya nyota wao wakisisitiza kuwa lazima kieleweke.
Wakizungumza na Mwanaspoti kwa nyakati tofauti, mashabiki wa timu hizo kila mmoja alitamba kuwa maandalizi waliyoyafanya ikiwamo usajili watatesa sana pale Ligi itakapoana.
Kibaraza Ramadhan ambaye ni shabiki wa kutupwa wa Simba, alisema timu yao imejiandaa vyema na wana matumaini ya kuendeleza moto kutokana na usajili wa maana walioufanya.
Alisema uwapo wa wachezaji, beki Joash Onyango, Luis Miquisone na Benard Morrison, lazima waendeleze heshima kwa kufanya kweli katika Ligi na kwamba matarajio yao ni kubeba tena makombe.
“Msimu uliopita kulikuwa na upungufu kidogo sehemu ya beki, lakini ujio wa Onyango tatizo limeisha inamaana akiwapo yeye, halafu Miquissone na Morrison lazima mtu afe nyingi,” alisema Kibaraza.
Kwa upande wake, Hashim Omary, shabiki kindakindaki wa Yanga, alisema usajili wa wachezaji Tuisila Kisinda na Michael Sarpong utawaliza wengi kwani kazi yao ilionekana katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Eagle Noir.
WALIVYOSAJILI
SIMBA: Wamewaacha wachezaji sita, Tairone Santos, Sharaf Eldin Shiboub, Shiza Kichuya, Haruna Shamte, Rashid Juma na Yusuph Mlipili ambao wote walikuwa hawapati nafasi ya kucheza mara kwa mara.
Wameingia saba ambao ni mabeki Joash Onyango na Ame Ibrahim, washambuliaji, Benard Morrison, Chris Mugalu na Charles Ilanfya.
Simba imemuongeza kiungo fundi, Larry Bwalya na David Kameta aliyekuja kumsaidia Shomary Kapombe baada ya kuachwa Shamte aliyekwenda Namungo.
YANGA: Wamewaleta makocha watatu, Zlatko Krmpotic na msaidizi wake Juma Mwambusi na Vladimir Niyonkuru wa makipa.
Imeboresha safu ya ulinzi kwa kuwaleta, Bakari Mwamnyeto, Yassin Mustapha, Kibwana Shomari na Abdallah Shaibu ‘Ninja’.
Wameletwa washambuliaji wapya, Waziri Junior, Farid Mussa, Carlos Fernandez ‘Carlinhos’, Michael Sarpong, Tuisila Kisinda na Sogne Yacouba. Yanga imeboresha eneo la kiungo kwa kumnasa Tonombe Mukoko, ambaye amekuja kuchukua nafasi ya Papy Tshishimbi.
Wamemchukua Senzo Mazingisa aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, ili kuongeza nguvu katika eneo la uongozi.
AZAM: Mabadiliko ambayo Azam, imeyafanya iliachana na kipa Razack Abalora ambaye nafasi yake ilichukuliwa na David Kisu na ilimchukua Emmanuel Charles ili kumsaidia beki wa kushoto Bruce Kangwa.
Katika kuboresha safu ya ushambuliaji iliwaleta, Alain Akono, Prince Dube, Ayoub Lyanga, Awesu Awesu na Ismail Aziz ambao wameaminiwa kwenda kuongeza makali ya eneo hilo.
NAMUNGO: Imempoteza mshambuliaji Reliants Lusajo kwasababu za kimasilahi. Imewasajili Sixtus Sabilo, Stephen Sey, Iddi Kipagwile na Shiza Kichuya.
Namungo ambao wamesajili wachezaji 11 kwenye dirisha hili kubwa imeongeza nyota wapya katika eneo la kiungo Abdulhalim Humoud na Fredy Tangalo. Safu yao ya ulinzi iliruhusu mabao 37 msimu uliopita imeboresha msimu huu kwa kuletwa Amani Kyata, Haruna Shamte, Jafar Mohamed , Frank Magingi na kipa Johnathan Nahimana.