HISIA ZANGU: Tuliogopa ubao wa matokeo ukisoma Yanga 1- Azam 3

WAAMUZI wetu hawajui? Au wanahongwa? Au wana mapenzi na timu kubwa? Maswali matatu muhimu katika kujiuliza kilichotokea kwenye pambano la juzi kati ya Yanga na Azam pale Temeke. Sina shaka majibu yote matatu ni sahihi.

Nimekaa katika mpira wa Tanzania kwa muda mrefu sasa kujua kwamba majibu yote sahihi. Inategemea tu na jinsi mwamuzi alivyochezesha mechi. Wakati mwingine jibu la kwanza ni sahihi zaidi kuliko mengineyo.

Tungeweza kuwa na mechi ambayo sasa tungekuwa tunasema Yanga amechapwa mabao matatu na Azam. Lakini sasa tunasema pambano liliisha suluhu. Tukiwapelekea Wazungu au mashabiki kutoka nje watashangaa sana.

Tunaanzia wapi? ‘Bao la kwanza’ la Azam lililofungwa kwa kichwa katika dakika ya pili tu ya mchezo na Never Tigere. Kona fupi ilianzishwa na Idd Nado. Walinzi wa Yanga wakawa wazito kutoka katika boksi lao. Aliyekuwa mzito zaidi alikuwa Jaffary Mohammed.

Alishuhudia Idd Nado akipiga krosi yeye akawa anatazama akiwa amesimama pale pale. Richard Djodi na Abdalah Heri wakaruka kwa pamoja wote wakiwa hawajaotea. Kheri akafunga kwa urahisi tu.

Najua kilichozungumzwa na watu waliokwenda uwanjani. Utasikia mtu anasema “Wawili hao peke yao, offside hiyo”. Tanzania bwana! Wachezaji wakibakia wawili au watatu peke yao wanatazama na golikipa hukumu ya kwanza ni kwamba wameotea. Haijalishi kama waliuvunja mtego wa kuotea.

Unaporudi katika bao hili unashangazwa na kitu kimoja. Mwamuzi Msaidizi alikuwa anawaza nini? Mchezaji ambaye alikuwa mzito kuondoka nyuma, Jaffary alikuwa karibu zaidi na mwamuzi msaidizi. Alikuwa katika upande wake. Kumbuka Jaffary alikuwa mlinzi wa kushoto na hilo linamfanya awe karibu na mwamuzi msaidizi ambaye anakimbizana na mstari ulio jukwaa kubwa wanapokaa mashabiki wa Yanga.

Mwamuzi msaidizi wa upande wa pili kule akakumbana tena na Jaffary wakati mpira ulipokwenda kipindi cha pili. Huyu alikuwa mzembe kwa uamuzi mbovu wa Jaffary wakati alimpokwatua Nicolas Wadada wakati alipoingia kwa kasi ndani ya boksi la Yanga.

Ilipaswa kuwa penalti. Lawama ya kwanza inakwenda kwa mwamuzi Heri Sasi. Sijui alikuwa anafikiria nini kuinyima Azam penalti. Labda atasema kuwa kulikuwa na miili mingi mbele yake na hakuweza kuiona ‘tackling’ ya ovyo ya Jaffary.

Hii sio sababu. Mwamuzi anapaswa kuwa mita 10 kutoka pale mpira unapodunda. Ukimweka kando Sasi unamgeukia mwamuzi msaidizi wa upande wa mashariki. Yeye anaruhusiwa kumrekebisha mwamuzi kama hakuona. Yeye alikuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kuona faulo ya Jaffary. Mbele yake hakukuwa na mchezaji yeyote wa kuziba nafasi yake tofauti na Sasi. Hakuchukua uamuzi wowote.

Ni huyu huyu pia ndiye ambaye angeweza kumsaidia mwamuzi na kuacha kunyoosha kibendera wakati Richard Djodi alipoingia katika boksi kwa kasi na kuvunja mtego wa kuotea na hivyo kumpasia Never Tigere aliyefunga kiulaini.

Kinachokera zaidi ni kwamba kwa mapana na marefu ya uwanja, licha ya kwamba Djodi alikuwa ndani ya boksi lakini aliingia kwa kupitia upande ule ule wa mwamuzi msaidizi wa upande wa mashariki. Kwanini hakuona? Ni Mungu pekee anajua.

Tusiwanyime haki Yanga. Nao walistahili penalti ambayo ingeweza kuwapatia bao la kufuatia machozi katika pambano la juzi. David Molinga alikatwa na Wadada katika boksi, mwamuzi alipeta. Wadada alimkwatua Molinga kwa mguu wa kulia, alipoona haitoshi akamkwatua kwa mguu wa kushoto. Ilipaswa kuwa penalti.

Mwamuzi alidhamiria pambano liishe kwa sare? Labda. Alidhamiria kusawazisha matokeo? Labda. Inawezekana Wadada alinyimwa penalti yake katika kipindi cha pili kwa sababu katika lango lile lile Molinga alinyimwa penalti yake?

Inawezekana Molinga angepewa penalti yake basi na Wadada angepewa penalti yake? Wakati mwingine waamuzi wetu wanatumia njia hii kwa sababu ya kujiweka katika sehemu salama zaidi kwa mashabiki wa pande zote.

Mambo hayakuwa mazuri kwa Sasi na wenzake juzi kwa sababu kulikuwa na mabao mengine mawili zaidi ambayo wangeweza kufunga. Matokeo yangesomeka 1-3. Hii ina maana kwamba hata balansi yao waliojitahidi kuifanya ilishindikana.

Waamuzi wanahongwa? Katika mechi kubwa inanishangaza kama mwamuzi anakubali kuhongwa ili apendelee timu fulani mbele ya maelfu ya mashabiki waliopo uwanjani, au mamilioni ya mashabiki wanaofuatilia katika televisheni kama pambano la Yanga na Azam lilivyofuatiliwa.

Katika dunia ya leo ya marudio ya televisheni unaweza kuharibu mechi ya soka inayotazamwa na mashabiki zaidi ya milioni mbili ndani na nje ya nchi? Kwa waamuzi wa juzi nadhani walishindwa tu kumudu kanuni za soka.

Kitu kikubwa ambacho tumeendelea kukosea ni ukweli kwamba Watanzania wengi tumejikita zaidi katika kuwalaumu waamuzi wa katikati. Wakati mwingine tunakosea. Waamuzi wa pembeni wanatoa mchango mkubwa sana kuharibu mechi kuliko waamuzi wa katikati.

Jaribu kutazama ukweli kwamba matukio mengi yanatokea huku mwamuzi akihitaji zaidi msaada kutoka kwa waamuzi wa pembeni lakini hapati msaada huo. Mwamuzi anajikuta akichezesha mechi kwa hisia zake peke yake.

Kwa mfano, pambano kati ya Simba na Yanga raundi ya kwanza, dada yenu Jonesia Nkya alikosa msaada wa mwamuzi msaidizi namba moja wakati alipotoa uamuzi wa penalti kwa Simba huku Kelvin Yondani akimvuta Meddie Kagere nje ya Boksi.

Mwamuzi msaidizi kazi yake ilimpaswa awe amesimama mstari mmoja na mtu wa mwisho ambaye alikuwa ni Meddie Kagere. Yeye alipaswa kuona vema kutokea pembeni kuliko Jonesia aliyetazama kutokea nyuma.