Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hisa za Simba : Wataalamu wafafanua mpango mzima ulivyo

Muktasari:

Lakini ukiachana na kauli hiyo ya serikali, wataalamu mbalimbali wa uwekezaji wametoa ufafanuzi juu ya utaratibu wa mfumo mpya ambao klabu ya Simba itauingia, baada ya kuuza asilimia 49 ya hisa kwa Mo Dewji.

JANA Jumatano, Serikali kupitia Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe imeeleza namna ambavyo klabu ya Simba iliyoingia kwenye mfumo wa kampuni wa hisa ikieleza jinsi mfumo unavyopaswa kuwa.

Dk Mwakyembe alisema mfumo wa hisa wa Msimbazi hauruhusu mwekezaji kuwa mmoja kama ambavyo ilikuwa ikifahamika na wengi kwa Bilionea Mohammed ‘Mo’ Dewji ndiye mwekezaji mwenye hisa asilimia 49, huku asilimia zilizosalia zinakuwa za klabu.

Serikali ilisema ilishatoa maelekezo ya nini kifanyike ili Simba kuingia kwenye mchakato huo kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lakini ni kama TFF ilizembea na sasa wameliacha jukumu hilo kwa Baraza la Taifa la Michezo (BMT).

Lakini ukiachana na kauli hiyo ya serikali, wataalamu mbalimbali wa uwekezaji wametoa ufafanuzi juu ya utaratibu wa mfumo mpya ambao klabu ya Simba itauingia, baada ya kuuza asilimia 49 ya hisa kwa Mo Dewji.

MPANGO UKO HIVI

Simba iliamua kufanya mabadiliko ya kuingia kwenye mfumo wa kisasa wa uendeshaji na kupitishwa kwenye Mkutano Mkuu wa klabu hiyo na kumtangaza Mo Dewji mwekezaji wao kwa asilimia 49 za hisa zenye thamani ya Sh20 bilioni.

Baada ya utaratibu kukamilika, maelfu ya wanachama wa klabu hiyo watamiliki asilimia 51 ya kampuni, huku Mo Dewji ambaye ni mwekezaji wa kimkakati atakuwa akishikilia majukumu makubwa ya maamuzi ya uendeshaji wa Simba.

Kwa utaratibu wa kawaida, mashabiki wengi na wadau wa mpira wamekuwa wakijiuliza ni kwanini Mo Dewji, ambaye yuko kwenye taratibu za mwisho kununua hisa kwenye klabu hiyo, atakuwa na nguvu za kimamlaka kwenye klabu dhidi ya wanachama wenye asilimia 51. Wataalamu wa masuala ya uwekezaji wamelifafanua hili.

Mpango wa Simba kuelekea kampuni huenda ukapunguza migogoro kwenye klabu hiyo kongwe nchini, ambayo ilianzishwa na wafanyabiashara maeneo ya Msimbazi - Kariakoo miaka 88 iliyopita.

Mo ambaye baada ya kukamilika kwa taratibu za ununuaji hisa atakuwa ndiye mwendeshaji wa klabu ya hiyo ya Simba, ambayo iliiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya Klabu Bingwa ya Afrika.

Kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi uliofanyika miezi kadhaa iliyopita, wanachama ambao wanamiliki asilimia 51 ya hisa wana wajumbe wanane, huku Mo ambaye anamiliki asilimia 49 akiwa na idadi hiyo hiyo ya wajumbe kwenye bodi.

KWANINI KUWE NA WAJUMBE SAWA?

Wataalamu wa masuala ya uwekezaji na hisa kwenye Masoko ya Mitaji wamesema kwamba suala la Simba na umiliki, na majukumu ya kuendesha klabu ni la kawaida na hakuna utaratibu wowote utakaovunjwa hata kwa kumpa Mo asilimia 50 ya maamuzi ya kampuni.

Mkurugenzi Mtendaji wa Orbit Securities, Washauri wa Uwekezaji kwenye Masoko ya Mitaji na Hisa, Juventus Simon anasema kwamba kwa kuwa Mo Dewji ni mwekezaji wa mkakati wa klabu hiyo na malengo yake ni kupata faida kutoka kwenye fedha alizowekeza, hayuko tofauti na wawekezaji wengine kwenye sekta nyingine za uchumi.

Anasema haoni shaka kuona Mo Dewji na wanachama wa Simba wakiwa sawa kwenye maamuzi yanayohusu klabu kwani kila kitu kinafanyika kwa kulingana na makubaliano yaliyofanywa kabla ya ununuaji wa hisa hizo.

“Mwekezaji mwenye hisa nyingi ama mwekezaji yeyote huwa anaanza na makubaliano kabla ya kuingiza uwekezaji wake wa fedha na suala la uendeshaji ama menejimenti huwa ni baadhi ya manufaa ya uwekezaji,” alisema Juventus.

Alitolea mfano wa benki ya NMB ambapo serikali inamiliki asilimia 31.78 na benki ya Rabo ya Uholanzi ikimiliki asilimia 34.9, lakini kwenye maamuzi huwa wanashirikiana na uendeshaji wa kampuni pia hupatikana kutokana na makubaliano ya hao wawekezaji wawili wenye hisa nyingi.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Zan Securities, Washauri wa Uwekezaji, Raphael Masumbuko anasema kwamba pale utaratibu utakapokamilika, ndipo taratibu za uendeshaji na menejimenti ya klabu zitakapofikiwa.

“Baadhi ya kampuni, kwa mwekezaji anapokuwa na hisa nyingi, basi yeye ndiye anakuwa na turufu kubwa kwenye maamuzi na uendeshaji, na huwa ana ushawishi mkubwa kwenye maamuzi ya kiutendaji,” alisema kwenye mazungumzo na Mwanaspoti.

“Iwapo Mo Dewji anakuwa na hisa 49, ambayo kimsingi ni kubwa na hisa zilizobaki zikiwa zinamilikiwa na wengine ambao wanamiliki hisa kidogo kidogo na hawakuungana kama taasisi au kampuni, basi hii itampa nafasi kubwa na kuwa ndiye mwamuzi mkuu wa masuala ya klabu,” anasema.

Anasema kwa kuwa wanachama wana hisa mbili zaidi ya zile za Mo Dewji, bado pengo hilo ni dogo sana na ni rahisi kuwa na ushawishi.

MFUMO WA KAMPUNI KWENYE SOKA

Baada ya kukamilika kwa taratibu, klabu ya Simba ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu Bara (TPL 2018/19) itakuwa ni ya kwanza kuingia kwenye mfumo wa kampuni.

Klabu nyingine inayoendeshwa kiuwekezaji mkakati ni Azam FC, ambayo ilianzishwa na Salim Said Bakhressa (SSB) na imekuwa ikifanya vizuri kwani haina migogoro kama klabu zinazoendeshwa na wanachama.

Klabu nyingine ya Yanga, ambayo ni mabingwa wa kihistoria Tanzania nayo ipo mbioni kuingia kwenye utaratibu kama huu, kwani awali walishawahi kuuanza lakini uliingia dosari kutokana na baadhi ya wajumbe kutokubali mfumo huo mpya wa kibiashara.

Ndani ya katiba yao, Yanga wameweka bayana mfumo wa kisasa ambao utaifanya iende na wakati ambapo soka limekuwa biashara na sio suala la kujiburudisha tu na hata klabu za Ulaya na nyingine za Afrika na Asia zimekuwa zikiendeshwa kisasa na kuvuna mamilioni ya fedha.