AFCON U-20: Ngorongoro Heroes kujiuliza kwa Sierra Leone

Muktasari:
- Timu hiyo inakutana na Sierra Leone inayoongoza kundi A ikiwa na pointi nne kwenye mechi mbili ilizocheza, ikitoka sare ya bila kufungana na Zambia huku ikiifumua Misri kwa mabao 4-1.
BAADA ya Timu ya taifa ya vijana 'Ngorongoro Heroes' kupoteza mechi ya kwanza ya kundi A kwenye kampeni za kusaka ubingwa wa Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 20 (Afcon U-20), leo Mei 3 itakuwa mzigoni kutafuta matokeo kwenye mchezo wa pili dhidi ya Sierra Leone utakaopigwa katika Uwanja wa Suez Canal, Ismailia nchini Misri.
Ngorongoro ilipoteza mechi ya kwanza dhidi ya Afrika Kusini kwa bao 1-0, matokeo yaliyoifanya kusalia mkiani ikiwa haina pointi.
Timu hiyo inakutana na Sierra Leone inayoongoza kundi A ikiwa na pointi nne kwenye mechi mbili ilizocheza, ikitoka sare ya bila kufungana na Zambia huku ikiifumua Misri kwa mabao 4-1.
Akizungumzia mchezo huo, Kocha wa Ngorongoro, Charles Mkwasa alisema wanafahamu ubora wa wapinzani na wameshafanyia kazi makosa ya kukosa nafasi kwenye mchezo uliopita.
"Tumelifanyia kazi suala la kupoteza nafasi. Tulikuwa bora mchezo uliopita, lakini mbele kidogo kulikuwa na changamoto. Naamini maagizo tuliyowapa (wachezaji) wameyafanyia kazi na kuhakikisha tunashinda," alisema Mkwasa.
Baada ya mchezo huo, Mei 6 Ngorongoro itaumana na Zambia na kumalizia ratiba ya makundi dhidi ya wenyeji kisha kusikilizia kama itafuzu robo fainali au la.
Fainali za Afcon U20 zinaendelea Misri zikishirikisha timu 13 zilizopangwa katika makundi matatu, na zilianza Aprili 27 zikitarajiwa kufikia tamati Mei 18, ambapo timu nne zitakazotinga nusu fainali zitakata tiketi ya fainali za Kombe la Dunia U20 zitakazofanyika nchini Chile.
Ngorongoro Heroes ilishiriki mashindano hayo kwa mara ya kwanza katika fainali za 2021, ambapo iliishia hatua ya makundi zilipofanyika Mauritania.
Misri ndio timu tishio zaidi katika kundi hilo kwa vile inashika nafasi ya pili kwa kutwaa taji mara nyingi ikifanya hivyo mara nne ambazo ni 1981, 1991, 2003 na 2013. Timu hiyo imeshika nafasi ya pili mara moja na iliwahi kumaliza katika nafasi ya tatu mara tatu.
Zambia ni timu nyingine iliyowahi kuonja mafanikio kwenye kundi A, ambapo imetwaa ubingwa mara moja ambayo ni 2017 na imewahi kushika nafasi ya nne mara tatu ambazo ni 1991, 1999 na 2007.
Mabingwa wa kihistoria wa fainali hizo Nigeria ambao wametwaa taji hilo mara saba, wamepangwa katika kundi B na timu za Tunisia, Kenya na Morocco. Mabingwa watetezi, Senegal wamepangwa Kundi C na Jamhuri ya Afrika Kati, DR Congo na Ghana.
Timu nne zinazotinga nusu fainali Afcon U20 zinajihakikishia tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia kwa vijana wa umri huo.