Himid, Sure Boy warudishwa Stars

Himid, Sure Boy warudishwa Stars

Muktasari:

  • Mastaa hao awali walikosekana kwenye kikosi cha mara ya mwisho kilichoitwa kucheza mechi ya za kirafiki za kalenda ya FIFA.

VIUNGO Himid Mao (Ghazi Mahl-Misri) na Salum Abubakari  ‘Sure Boy’ wa Yanga wamejumuishwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa Tanzania kinachoingia kambini kujiandaa na Fainali za Mataifa Afrika (AFCON) 2023.

Stars inaingia rasmi kambini Mei 28 kwa ajili ya mechi mbili za kufuzu AFCON dhidi ya Niger utakaopigwa nchini humo Juni 4 kisha watacheza na Algeria Juni 8 katika uwanja wa Benjamin Mkapa.

Wachezaji hawa awali hawakujumuishwa kwenye kikosi kilichocheza mechi ya za kirafiki za kalenda ya FIFA.

Akizungumzia kuitwa kwa wachezaji hao, kocha msaidizi wa timu ya Taifa Tanzania ‘Taifa Stars’, Shadrack Nsajigwa amesema sababu ya kuitwa kwa wachezaji hao ni kutokana na viwango wanavyovionyesha kwenye klabu zao.

Nsajigwa amesema kuingia kwa Mao na Sure Boy kwenye timu hiyo wamechukua nafasi za wengine ambao hawajaitwa.

“Mao na yeye licha ya awali alikuwa haitwi safari hii tumemuita kwa sababu watu wetu wamemfuatilia anachokifanya na kulizika na uwezo wake,” amesema Nsajigwa na kuongeza;

“Hatujamuita kwa sababu ya maneno ya mtandaoni bali tumemuita kulingana na kitu anachokifanya kwenye klabu yake.”

Wachezaji walioitwa ni Aishi Manula, Abuutwalib Mshery, Metacha Mnata, Shomari Kapombe, Kibwana Shomari, Haji Mnonga, Mohammed Hussein ‘Tshabalala ‘ na Nickson Kibabage.

Wengine ni Bakari Mwamnyeto, Dickson Job, Kennedy Juma, Abdallah Kheri ‘Sebo’, Novatus Dismas na Mzamiru Yassin.

Wengine ni Aziz Andambwile, Himid Mao, Simon Msuva, Kelvin John, Mbwana Samatta, Farid Mussa na Abdul Suleiman.

Wengine ni Feisal Salum, Ben Starkie, Reliants Lusajo, Kibu Denis, George Mpole, Salum Abubakari ‘Sure Boy’ na Ibrahim Joshua.