Hii ndio...! Yanga mpya ya Chama

Hii ndio...! Yanga mpya ya Chama

BALAA hilo. Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu ya Yanga, Senzo Mbata amethibitisha kuwasiliana na klabu ya Berkane Morocco kuulizia uwezekano wa kunasa huduma ya kiungo fundi wa mpira, Clatous Chama.

Wakati dirisha la usajili Ligi Kuu Tanzania Bara likifunguliwa Desemba 15, Senzo alisema: “Chama ni mchezaji bora hakuna klabu ambayo itakataa kuwa naye. Kwa sasa ana mkataba Berkane na tunaheshimu hilo. Lakini ni kweli tumeulizia uwezekano wa kumpata na kama kutakuwa na uwezekano wa kumleta basi tutamleta.”

Chama ana msimu mmoja tu tangu alipoondoka katika Ligi Kuu Bara, alipokuwa akikipiga kwenye kikosi cha Simba, ambao ni mahasimu wakubwa wa Yanga. Kama dili hili litatiki basi Chama ataingia kwenye orodha ya mastaa waliopata nafasi ya kucheza Simba na Yanga. Hata hivyo, ujio wa Chama Yanga utakuwa na maana gani kutokana na timu hiyo ilivyosheheni mastaa wa maana kwa sasa.

Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi na msaidizi wake, Cedric Kaze watakuwa na shughuli pevu katika upangaji wa kikosi, huku ujio wa Chama huko Jangwani utawapa mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu Tanzania Bara machaguo manne tofauti ya kiuchezaji ndani ya uwanja.

Mwanaspoti linachambua fomesheni nne ambazo Yanga inaweza kuzitumia kwa faida ya kuwa na mchezaji Chama kwenye kikosi chao.


Chaguo la Kwanza: 3-5-2 (Bangala anarudi nyuma)

Kocha Nabi anaweza kuwa na chaguo la kutumia mfumo huu wa kutumia mabeki wa kati watatu, ili kuongeza wingi wa wachezaji kwenye sehemu ya kati ya uwanja, huku akipata nafasi ya kuwa na orodha karibu yote ya wachezaji wake wa kikosi cha kwanza cha sasa licha ya kuwapo kwa ingizo jipya la Chama kwenye timu. Kwenye mfumo huu, Yannick Bangala atarudi kucheza beki ya kati sambamba na Dickson Job na Bakari Mwamnyeto. Langoni kama kawaida ataendelea kuwa kipa Djigui Diarra. Mastaa watano kwenye eneo la katikati, Kibwana Shomari na Djuma Shaban watacheza wing-back kushoto na kulia mtawalia, huku viungo watatu wa kati watakuwa Khalid Aucho, Mukoko Tonombe na Chama - wakati kwenye fowadi ya wakali wawili, kutakuwa na Feisal ‘Feitoto’ Salum na Fiston Mayele. Mfumo huu utawakosa mastaa wawili tu, ambao wamekuwa chaguo la kwanza la kocha Nabi msimu huu, ambao ni Jesus Moloko na Yacouba Songne.


Chaguo la Pili: 4-2-3-1 (Chama la ushindi)

Kwa mechi kadhaa ilizocheza Yanga kwenye Ligi hadi sasa, benchi la ufundi la vinara hao wanaonekana kupendelea mfumo huu zaidi wa kucheza 4-2-3-1, uliowaletea matunda makubwa na kushinda mechi zote tano za kwanza. Mfumo huo unakuwa na viungo wawili wa kukaba, Bangala na Aucho na umekuwa na matunda makubwa, ambapo katika dakika 450 ilizocheza Yanga kwenye ligi hadi sasa, imeruhusu wavu wao kuguswa mara moja tu. Kwenye fomesheni hii, Yacouba ataanzia benchi, huku kuanzia langoni, Diarra atapata nafasi yake na kulindwa na ukuta wa mabeki wanne, Kibwana kushoto, Djuma kulia na Mwamnyeto na Job watasimama katikati. Kwenye safu ya mastaa watatu watakaocheza nyuma ya mshambuliaji wa kati, Mayele, Chama atakuwa upande wa kushoto, Feitoto Namba 10 na Moloko atakimbiza upande wa kulia. Timu ya mafundi watupu.


Chaguo la Tatu: 4-1-4-1 (Feisal benchi)

Kocha Nabi na benchi lake la ufundi wamekuwa na utaratibu wa kumfanya kiungo Feitoto kuachwa kucheza kama mchezaji huru kwenye Namba 10, lakini ujio wa Chama unaweza kumfanya kiungo huyo wa kimataifa wa Tanzania akapata muda wa kupumzika na si kuchezeshwa kila mechi. Kwenye mfumo huu, Aucho atasogea kwa juu kidogo, akisimama kwenye mstari wa mastaa wanne nyuma ya mshambuliaji wa kati, ambapo wakali wengine hapo watakuwa Yocouba upande wa kulia, Moloko kulia na Chama atacheza Namba 10, akiwa nyuma ya mshambuliaji wa kati, anayeweza kuwa, Mayele au Heritier Makambo. Ukuta utabaki na wakali walewale wanne, Kibwana, Mwamnyeto, Job na Djuma, huku mbele yao kwenye safu ya kiungo ya kukaba, kutakuwa na Bangala.


Chaguo la Nne: 4-3-3 (Kumiliki mpira muda wote)

Ujio wa Chama utamfanya Nabi kuwa na kikosi chenye mastaa wengi wenye uwezo wa kumiliki mpira. Kwa staili ya soka la kupiga pasi nyingi ndani ya uwanja, fomesheni ya 4-3-3 inaweza kuwa chaguo sahihi kwa benchi hilo la ufundi la miamba hiyo ya Jangwani. Kwenye fomesheni hii, langoni atabaki kuwa Diarra, akilindwa na ukuta wa mabeki Kibwana upande wa kushoto, Job na Mwamnyeto wakisimama kati, huku Djuma akiwa kulia. Kati viungo watatu kutakuwa na Bangala, Aucho na Chama, huku ile safu ya wakali wa mbele kutakuwa na Feitoto, Mayele na Moloko. Nabi na benchi lake la ufundi wanaweza kutumia mfumo huo wa kiuchezaji kwenye mechi zenye ushindani mkali wa kumiliki mpira ndani ya uwanja.


WASIKIE WADAU

Nyota wa zamani wa Yanga, Ally Mayay na Pascal kaliasa walisema kama Chama itajiunga na Yanga, basi ni aina ya mchezaji atakayeenda na falsafa ya kocha Nabi.

“Nabi ni muumini wa falsafa ya kuuchezea mpira, ukimuona kocha beki yake inacheza pasi sita mpaka saba katika eneo lao na hana presha wala kuinuka, maana yake ndivyo aliwafundisha,” alisema Mayay na kuongeza, Chama ataenda kuongezea kitu katika umiliki wa mipira katikati ya uwanja, akitengeneza kombinesheni kali na Aucho na Feitoto, japo alisema eneo litakaloathirika na ujio huo ni la pembeni kwa kina Moloko akiamua kuchezes viungo wengi na Kaliasa alisema ujio wa Chama Yanga utatengeneza kombinesheni kali eneo la katikati.