Hersi, Arafat, Ibwe wajitosa CCM kuwania ubunge

Muktasari:
- Hersi amechukua fomu za kuwania ubunge katika Jimbo la Kigamboni jijini Dar es Salaam, huku Ibwe akijitosa kuwania ubunge kupitia Jimbo la Mwanga mkoani Kilimanjaro, ambako ndiko alikozaliwa.
RAIS wa Yanga, Hersi Said, Makamu wake Arafat Haji na Ofisa Habari na Mawasiliano msaidizi wa Azam FC, Hasheem Ibwe, leo Juni 28, wamejitosa kuchukua fomu za kuwania kuteuliwa kugombea ubunge kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyia Oktoba, mwaka huu.
Hersi amechukua fomu za kuwania ubunge katika Jimbo la Kigamboni jijini Dar es Salaam, huku Ibwe akijitosa kuwania ubunge kupitia Jimbo la Mwanga mkoani Kilimanjaro, ambako ndiko alikozaliwa.
Hersi ni miongoni mwa watu maarufu katika tasnia ya michezo kutokana na uongozi wake ulioipa mafanikio makubwa Klabu ya Yanga kwa kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara nne mfululizo tangu aliposhinda urais wa kikosi hicho, Julai 9, 2022.
Pia, Hersi ni mwenyekiti wa Umoja wa Klabu Afrika (ACA), huku upande wa Ibwe ni mwanahabari kitaaluma ambaye amebobea kwa zaidi ya miaka 10 na kashiriki shughuli mbalimbali za CCM.
Mbali na Hersi pia Makamu wa Rais wa Klabu ya Yanga, Arafat Haji amechukua fomu ya kugombea ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Shaurimoyo visiwani Zanzibar leo Jumamosi Juni 28, 2025.
Mbali na kuwa kiongozi kwenye klabu hiyo yenye maskani yake Jangwani, Dar es Salaam, Arafat pia ni Mkurugenzi wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ).
Akizungumza na Mwanaspoti baada ya kuchukua fomu hiyo, Ibwe amesema amefikia uamuzi wa kuwania ubunge huku akishukuru uongozi wa Azam FC kumpa sapoti na kumuunga mkono kutokana na kile alichokusudia.
"Nimekuwa CCM kuanzia mwaka 2005, nilipoanzia chipukizi Temeke jijini Dar es Salaam, ambapo hiyo tunaweza kuiita akademi kwenye mpira wa miguu, ilipofika mwaka 2010 ndipo nilichukua rasmi kadi yangu na kuwa mwanachama hai," amesema Ibwe.
Ibwe amesema licha ya wengi kushangaa kuwania nafasi hiyo, lakini hilo kwake hajali kwa sababu anachoangalia ni kile anachopenda.
"Hata viongozi wangu wa Azam FC walipojua nimeweka nia ya kugombea waliniunga mkono kwa sababu wanaamini katika malengo ya kila mmoja wetu. Nimekuwa nikifanya kazi ya tasnia ya habari na wakati huohuo nafanya shughuli za chama chetu pia," amesema.