Hersi anogesha shangwe la Yanga Msimbazi, bao la Chama...
Muktasari:
- Katika paredi hilo la Yanga linalofanyika leo Jumamosi Julai 4, 2026, lilianza mitaa ya Karume saa 7:00 mchana, ingawa lilipofika mitaa ya Msimbazi saa 8:00 mchana ambapo ndio makao makuu ya watani zao wa jadi, Simba ndipo ilipoibuka shangwe baada ya Hersi kujitokeza na kushangilia na mashabiki wa timu hiyo waliojitokeza kwa wingi.
RAIS wa Yanga, Injinia Hersi Said ameibua shangwe katika mitaa ya Msimbazi wakati timu hiyo ikiendelea na paredi la ubingwa wa Ligi Kuu Bara iliochukua kwa mara ya tano mfululizo.
Katika paredi hilo la Yanga linalofanyika leo Jumamosi Julai 4, 2026, lilianza mitaa ya Karume saa 7:00 mchana, ingawa lilipofika mitaa ya Msimbazi saa 8:00 mchana ambapo ndio makao makuu ya watani zao wa jadi, Simba ndipo ilipoibuka shangwe baada ya Hersi kujitokeza na kushangilia na mashabiki wa timu hiyo waliojitokeza kwa wingi.
Hersi aliibuka katika gari maalumu lililoandaliwa kwa ajili ya padre hilo na kushangalia huku akiwa na makombe matano iliyotwaa timu hiyo ya Ligi Kuu Bara.
Hata hivyo, licha ya Yanga kuteka shoo hiyo kwa kushangilia baadhi ya nyimbo mbalimbali za timu hiyo, ila mashabiki wa Simba hawakuwa nyuma kwani walijibu mapigo na kuimba pia nyimbo za kikosi hicho, ikiwemo ya Tunda Man ya Simba tambeni.
Katika mitaa ya Msimbazi ndipo yalipo makao makuu ya Simba, ambapo Yanga inatumia sehemu hiyo kuwakejeli kila ikifika eneo hilo baada ya kukosa ubingwa wa Ligi Kuu kwa mara ya tano mfululizo.
Bao la Chama lapamba paredi la Yanga
WAKATI Yanga ikisherehekea paredi la ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya tano mfululizo, mashabiki wa Simba wamezidi kujifariji kwa bao lililofungwa na nyota wao Clatous Chama katika mechi ya'Kariakoo Derby', ya Mei 3, 2026.
Hali hiyo imejitokeza katika mitaa ya Msimbazi wakati Yanga iliposimama kwa ajili ya kusherehekea ubingwa huo ikiwa ni njia ya kuwakejeli watani zao wa jadi, Simba ambao imekosa taji hilo kwa mara yake ya tano mfululizo.
Wakati Yanga ilipowasili mitaa ya Msimbazi, kulikuwa na skrini kubwa iliyokuwepo ambapo ilitumika kwa ajili ya kuonyesha bao la Chama ikiwa ni njia ya kujibu mapigo kutokana na mashabiki wa Yanga kushangilia taji hilo katika maeneo hayo ya Msimbazi.
Katika mechi ya Ligi Kuu Bara kati ya timu hizo maarufu 'Kariakoo Derby', Chama alifunga bao kwa staili ya tiki-taka likiwa ni miongoni mwa mabao bora, yanayopigiwa chaguo ya kushinda bao bora la msimu wa 2025-2026.
Mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo Mbweni, jijini Dar es Salaam, Mei 3, 2026, iliisha kwa miamba hiyo kutoka sare ya mabao 2-2.