Bodi ya Ligi Zanzibar kuwabana wanaopanga matokeo
Muktasari:
- Akizungumza na Mwanaspoti, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Zanzibar, Issa Kassim Ali, alisema ili kukomesha mambo hayo, wamezungumza na vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa jambo hilo.
BAADA ya kumalizika kwa Ligi Kuu Zanzibar msimu wa 2025-2026, kati ya mambo yaliyoitikisa ligi hiyo ni upangaji wa matokeo jambo ambalo limeonekana kuichafua ligi hiyo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Zanzibar, Issa Kassim Ali, alisema ili kukomesha mambo hayo, wamezungumza na vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa jambo hilo.
Alisema, baada ya uchunguzi huo kukamilika, hawatasita kuwachukulia hatua za kinidhamu kwa mujibu wa kanuni wale wote watakaobainika kuhusika.
“Zanzibar kuna uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya michezo, hivyo kuwa na vitu kama upangaji wa matokeo haitoleta picha nzuri duniani na watakuwa wanadumaza juhudi za Serikali,” alisema.
Pia, alisema wamefarijika kuona vyombo vya usalama vimekuwa tayari kutoa ushirikiano juu ya hilo, hivyo wanachosubiria ni matokeo ya uchunguzi huo.
Mtendaji huyo, alisema Bodi haiwezi kutoa adhabu ya moja kwa moja kuhusiana na suala la upangaji wa matokeo bila ya kupata ushahidi uliojitosheleza.
Alisema, ni ngumu kuibaini moja kwa moja nani anahusika na upangaji wa matokeo kama haujafanyika uchunguzi wa kina kulingana na matukio yanayojiri.
Kassim alisema kuelekea msimu ujao, Bodi hiyo itakaa na viongozi wa timu kutathmini kwa pamoja uendeshaji wa ligi na kutafuta mwarobaini wa changamoto zitakazobainika.
Alieleza kuwa, mbali na hilo Bodi hiyo imejipanga kuzungumza na kamati ya waamuzi ili kutoa mafunzo zaidi ya kuzitafsiri vyema sheria 17 za mpira wa miguu kwa lengo la kuepuka makosa madogomadogo kwenye mchezo.