HAWA TUMEWAONA, TUWASUBIRI NA WALE

Muktasari:
Wachezaji wapya wa kigeni wa Simba, wote tumeshawaona, kwahiyo hatuna deni na hao hadi sasa. Bado mchezaji mmoja wa Azam FC, Allan Thierry kutoka Cameroon na wachezaji wa kigeni wa Yanga
KIPINDI kikubwa cha usajili cha msimu huu kimechangamka kupita vipindi vyote vilivyotangulia katika miaka ya hivi karibuni.
Sakata la Morrison kwa Yanga na Simba. Sakata la Salum Abubakary ‘Sure Boy’ kwa Azam FC na Yanga. Sakata la Larry Bwalya kwa Yanga na Simba.
Bila kusahau sakata la Yanga na waandamizi wao, Juma Abdul, Tshishimbi na Kelvin Yondani, na masakata mengine mengi ambayo aidha hayakupata muda wa kutosha wa hewani, au hayakupata kabisa, japo yalikuwa makubwa.
Mbwembwe za basi la Azam FC na baadaye ndege yao ilipozunguka huku na huko kukusanya wachezaji wa kukiongezea nguvu kikosi cha matajiri hao wa jiji.
Baada ya masakata haya kwenye vyombo vya habari, sasa yanatakiwa kubadilishwa na kuwa viwango halafu yahamishiwe uwanjani.
Hakuna mwenye shaka na Bernard Morrison kwa sababu alishathibitisha katika miezi yake 6 ya kwanza akiwa Yanga.
Hakuna mwenye shaka na wachezaji wazawa ambao wametoka klabu za hapa nchini au hata nje ya nchi kama kipa wa Azam FC, David Mapigano ‘Kissu’, viungo wa Yanga, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na Farid Mussa, kwa sababu tayari tunawajua.
Sisi tunataka kuona wachezaji wa kimataifa waliosajiliwa kwa mbwembwe msimu, je yaliyomo yamo?
Wikendi iliyopita imeshuhudiwa timu mbili zilizofanya usajili wa mbwembwe zikitambulisha vikosi vyao kwa Watanzania, na tumeviona.
Kikubwa ni kwamba tumeona baaddhi ya wachezaji wao wa kigeni na kuwathiminisha kwa uwezo wetu wa Kitanzania.
TUMEWAONA
Sisi ni watu ambao tumeshuhudia wachezaji wetu wa kimataifa wakija nchini na kufanikiwa au kukwama, hivyo hatuwezi kukosa cha kusema kwa hawa ambao tayari tumewaona hadi sasa.
JOASH ONYANGO- SIMBA SC
Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Kenya kwa msimu wa 2018/19, Joash Onyango anaongeza uzoefu kwenye kikosi cha Simba.
Japo uchezaji wake na yawezekana hata umri wake hautofautiani sana na Serge Wawa, lakini anajua kujiweka kwenye nafasi na ni mzuri kumkabili mpinzani akiwa anamtazama.
LARRY BWALYA - SIMBA SC
Fundi mwingine aliyeongezeka kwenye idara ya kiungo ya Simba na kuongeza presha kwa kina Ibrahim Ajib.
Ana uwezo kupiga pasi ndefu kama za Jonas Mkude, Mudathir Yahya au Frank Domayo.
Kama alivyo Chama au Ajib, Larry ni mchezaji mzuri pale timu yake inapoutawala mchezo na kuwa na asilimia kubwa wa umiliki.
Mchezo unapotawaliwa na wapinzani, siyo mzuri wa kuziba nafasi na kuwatia presha wapinzani kwa kuwakaba.
CHRIS MUGALU - SIMBA SC
Mkongo kutoka Zambia ambaye hakuwa na msimu mzuri wa 2019/20 kutokana na majeraha.
Ni mzuri zaidi anapokuwa karibu au ndani ya kisanduku cha hatari.
Ni aina ya Bocco au hata Kagere, siyo mtu wa udambwidambwi sana, lakini faida kubwa kwake ni kuwa na nguvu na nia ya kujaribu zaidi na zaidi.
ALLY NIYONZIMA - AZAM FC
Idara ya kiungo cha chini ni miongoni mwa idara chache kiwanjani ambazo zimeshuhudia ubunifu mkubwa wa kiufundi.
Kutoka half ‘back six zamani’ hadi kuwa na holding, defensive na hata deep lying midfielders.
Ally Niyonzima anacheza zaidi kama holding midfielder (kiungo mtuliza timu) badala ya defensive midfielder (kiungo wa ulinzi au mkata umeme) au deep lying midfielder (kiungo kuendesha timu kutokea chini).
Ana utulivu sana akiwa na mpira, anafika kwa wakati na anajua kutumia umbo lake refu kwa kucheza mipira ya juu na kuingiza miguu yake kwa mpinzani anayeonekana yuko mbali kidogo.
Lakini zaidi anajua kuanzisha mashambulizi kwa pasi fupi fupi na ndefu.
Endapo kocha wa Azam FC, Aristica Cioaba, atamtumia kama ninavyomuona mimi, yaani holding midfielder, halafu akamuweka Novatus Dismas kama typical defensive midfielder (kiungo halisi wa ulinzi) kisha juu yao akawekwa Sure Boy, hakuna timu itakayotawala kiungo cha Azam FC msimu huu.
PRINCE DUBE - AZAM FC
Nchini Zimbabwe, Prince ni mmoja wa wachezaji wanaozungumzwa sana kwamba wana kesho yenye mafanikio.
Lakini kukaa nje ya uwanja kwa takribani miezi 9, siyo kitu rahisi kwa mchezaji.
Ligi ya Zimbabwe huanza mwezi Machi na kuisha Novemba au Disemba.
Kwa hiyo ligi ya msimu uliopita iliisha Disemba 2019, na ligi mpya ilipaswa kuanza Machi mwaka huu...lakini mlipuko wa maradhi ya COVID 19 yakasitisha msimu hadi sasa.
Kwa hiyo hajacheza mpira kwa kipindi chute hicho, asingeweza kuonesha uwezo mkubwa...na ndiyo maana hata kocha wake alimpa dakika chache za mwisho.
Lakini mchezaji mzuri huonekana anapopokea mpira wake wa kwanza tu. Kwa Prince Dube Azam FC wamepata mtu.
TUNAWASUBIRI
Wachezaji wapya wa kigeni wa Simba, wote tumeshawaona, kwa hiyo hatuna deni nao hadi sasa.
Bado mchezaji mmoja wa Azam FC, Alain Thierry Akono kutoka Cameroon na wachezaji wote wa kigeni wa Yanga.
Mukoko Tonombe
Tuisila Kisinda
Carlinhos Carmo
Yaccouba Sogne
Michael Sarpong
Tunawasubiri tuwaone.
Yaliyomo yamo?