Hata Ruvu nao kupanda ndege

Wachezaji wa Ruvu Shooting.

SAA chache baada ya kujihakikisha kusonga mbele katioka michuano ya Kombe la Shirikisho (ASFC) na huku wakiwa nafasi nzuri kwenye Ligi Kuu Bara, imewafanya Wazee wa Kupapasa, Ruvu Shooting kuanza kuota uwakilishi wa nchi kwa kutamani nao kupanda ndege kama wenzao.

Ruvu chini ya Kocha Boniface Mkwasa imeonekana kuwa ya moto katika michuano inayoshiriki msimu huu ikiwa nafasi ya tano katika Ligi Kuu Bara na alama zao 31, huku ikitangulia mapema hatua ya 16 Bora ya ASFC.

Vijana wa Masau Bwire, juzi ilikuwa kibaruani kupepetana na Mbao na kuing’oa kwa mabao 3-2 na kuwapa jeuri zaidi kwa kiamini huenda msimu ujao nao wakapanda ndege kuiwakilisha nchini.

Kocha Msaidizi wa Ruvu, Rajab Mchema alisema matokeo waliyonayo sio mabaya sana na malengo yao ni kumaliza ndani ya Nne Bora ya Ligi Kuu na kubeba ASFC ili waiwakilishe nchi.

Alisema kwa mwenendo mzuri wa Simba na Namungo katika ushiriki wao, inaweza kuwapa neema ya kushiriki michuano ya kimataifa na kwamba msimu ujao wanatamani kupanda ndege.

“Kwanza tunafurahi kufuzu hatua ya 16 bora ya kombe la shirikisho, malengo yetu tufike fainali lakini kwenye Ligi Kuu tunasaka zile nafasi nne za juu ili kufikia ndoto zetu hata kushiriki kimataifa” alisema Mchema.

“Katika mechi tatu, tumeshinda mbili ikiwamo hii ya FA, tumepoteza mmoja lakini siyo mbaya, tunaenda kujipanga upya na mechi zinazofuata kuhakikisha tunafanya vizuri” alisema Kocha huyo anayependa mchezo wa kasi na kupiga pasi fupifupi.