Hassan Kessy kaishika Zambia,ukisimuliwa mgogoro wa familia yake utalia

Muktasari:
Mwanaspoti ilizitembelea familia za wanasoka wanaotoka mkoani Morogoro, ambapo leo inakupa makala ya Kessy baada ya kuzungumza na familia yake, bibi Rehema Kessy na Moshi Mohamed Kingunde pamoja na baba yake mzazi Hamis Ramadhan Mzee ‘Kidingile’ mchezaji wa zamani wa Pamba FC ya Mwanza.
BEKI wa kulia wa Nkana FC ya Zambia na timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Hassan Ramadhan Kessy ni miongoni mwa nyota walioibuliwa na kituo cha Moro Kids kilichopo Morogoro. Kituo hiki kimewatoa wachezaji wengi kama Shomary Kapombe, Juma Abdul, Shiza Kichuya na wengine kibao.
Baada ya kuonyesha uwezo mkubwa, uongozi wa Moro Kids kama kawaida yao ulifanya mazungumzo na wenzao wa Mtibwa Sugar kwa lengo la kumsajili Kessy kwenye timu yao ya vijana ili kuanza kupata uzoefu.
Mtibwa Sugar walimsajili Kessy msimu wa 2011 aliitimikia timu hiyo hadi mwaka 2014, ndipo Simba walipomuona baada ya kucheza mechi ya Ligi Kuu ambayo kocha Mecky Mexime alimtumia na kuonyesha kiwango kikubwa.
Alitua Simba msimu wa 2014 kwa mkataba wa miaka miwili ambapo, hakupata changamoto ya namba kwani aliyekuwepo kwa wakati huo, Emiry Nimubona, raia wa Burundi hakuwa kwenye kiwango bora.
Msimu wa mwisho mwa 2016, Kessy alijiunga Yanga kwa mkataba wa miaka miwili ambao, ulimalizika mwaka jana, 2018 na kujiunga Nkana Rangers ya Zambia inayoshiriki Ligi Kuu nchini humo kwa mkataba wa miaka miwili. Akiwa Nkana ameshiriki michuano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.
Mwanaspoti ilizitembelea familia za wanasoka wanaotoka mkoani Morogoro, ambapo leo inakupa makala ya Kessy baada ya kuzungumza na familia yake, bibi Rehema Kessy na Moshi Mohamed Kingunde pamoja na baba yake mzazi Hamis Ramadhan Mzee ‘Kidingile’ mchezaji wa zamani wa Pamba FC ya Mwanza.
ALIPENDA SOKA KULIKO SHULE
Hassan Kessy ambaye kwa sasa amekuwa staa mkubwa pale Nkana, amekulia mkoani Morogoro na kusomea huko pia.
Hata hivyo, imeelezwa kuwa akiwa darasa la nne Shule ya Msingi Kikundi iliyopo mjini Morogoro, Kessy aliacha shule na kujikita katika soka kwani aliupenda zaidi.
“Shule alisoma hadi darasa la nne, Shule ya Kikundi. Baba yake hakuweza tena kumwendeleza ilibidi mtoto aendelee kuchezacheza mpira. Alianzia Moro Kids, alikuwepo hapo hadi anakwenda Mtibwa Sugar, lakini kabla ya hapo alikwenda kituo cha Uhuru akawa anasoma lugha ya Kiingereza huko Dar es Salaam.
“Akiwa Mtibwa Sugar ndipo Simba walimuona na kumchukua. Aliacha kusoma si kwa kupenda mwenyewe ila mzazi wake alishindwa kumwendeleza mwanaye.
“Baada ya baba yake kushindwa kumwendeleza kimasomo hata sisi tulishindwa kufanya lolote tuliona aendelee kufanya kile anachokipenda. Pale Mtibwa ndipo alipozaliwa Kessy na amekulia pale, alipoenda Mtibwa alitokea pale pale kwa bibi yake,” alisema Bibi Moshi.
MAFANIKIO
Ukifika nyumbani kwa kina Kessy utakuta nyumba ya zamani, ambazo sio za kisasa lakini ni imara.
Bibi Moshi anasema mjukuu wake alikuwa na mpango wa kuwabadilishia mjengo huo, lakini baadaye mambo hayakukaa vizuri.
“Kuhusu mafanikio yake zaidi kupitia soka sijafahamu kiundani ingawa nasikia anajenga Dar es Salaam ila sina uhakika kama ni kweli. Huenda mama yake mzazi anamshirikisha mambo yake mengine ya maendeleo.
“Tulikuwa tunamhurumia, tulimwacha apumue maana alivyoondoka Simba alikuwa na matatizo mengi, hivyo isingekuwa rahisi kuanza kumbebesha mzigo mwingine kwa ajili yetu, Kessy anafahamu alikotoka na sasa amekuwa mkubwa basi ipo siku atajua nini cha kuifanyia familia yake, anafahamu alikotoka na maisha yake kwa ujumla.”
Imeelezwa kuwa alitaka kuibomoa nyumba ili ajenge nyumba ya kisasa. Hiyo ikiwa ni moja ya kutoa shukrani kwa familia yake iliyomlea hadi alipofika sasa.
“Kulikuwa na matatizo la kiwanja pale kwa bibi yake, matatizo ya kodi ya ardhi alitoa Sh 300,000 nilikwenda kulipia mwenyewe, halafu alitaka kujenga nyumba ya kisasa ile ya zamani iondolewe, tulipiga mahesabu ya kuanza ujenzi, lakini baadaye mambo yakabadilika. .
Kwangu Kessy ni kijana mwenye busara ndiyo maana hata aliponunua kiwanja chake Dar aliniambia ingawa sijui maendeleo,” anasema bibi Moshi.
FAMILIA YARIDHIA KUACHANA NA SIMBA
Akiwa Simba aliingia kwenye mgogoro na viongozi wake ambao, ulianzia kwenye madai yake ya usajili pamoja na ahadi alizokuwa amepewa ikiwemo nyumba ya kuishi. Mgogoro huo ulisababisha Kessy kujiengua kikosini na kurudi kwao Morogoro hiyo ikiwa ni njia ya kushinikiza alipwe chake kama walivyokubaliana.
Baada ya kutekelezewa mahitaji yake, Kessy alirejea kwenye timu ingawa mambo yalikuwa magumu kwake kwani ile imani kwa mashabiki wa Simba pamoja na viongozi ilianza kupotea, hawakumwamini kwa asilimia 100 kama ilivyokuwa awali.
Ilifikia wakati hata aliyekuwa kipa wa Simba, Vincent Angban, raia wa Ivory Coast alimzaba vibao Kessy, lakini uongozi walilinyamazia yote hayo ilikuwa kama wamekasirishwa na uamuzi aliokuwa ameufanya beki huyo.
Kessy aliamua kutimkia Yanga wakati mkataba wake umebaki mwezi mmoja tu. Ilikuwa ni baada ya kumalizika msimu wa ligi ambapo kikanuni mchezaji anaruhusiwa kufanya mazungumzo na timu nyingine endapo mkataba wake utakuwa umebaki miezi sita.
Kessy alibakiza mkataba wa mwezi mmoja na Simba ndipo alipozungumza na Yanga ikiwemo kumalizana, kitendo hicho hawakukikubali waliamua kufungua kesi Shirikisho la Soka (TFF) ambapo Kessy na Yanga walilazimika kuilipa Simba Sh 50 milioni kwa madai ya kuvunja mkataba bila makubaliano yoyote.
Hiyo ni misukosuko mikubwa aliyokumbana nayo Kessy kwenye soka ingawa alipoondoka Yanga kwenda Nkana ya Zambia mkataba wake na Yanga ulimalizika na hawakuwa na pesa ya kumpa ya kusaini wakati wanataka kumwongeza mkataba, hivyo waliruhusu aondoke kwenda kujaribu maisha kwingineko.
Bibi Mosha anaelezea sakata hilo na kwamba, walibariki mjukuu wao kuiacha Simba kwani walihofia angepata matatizo.
“Katika mgogoro wa Simba tulimruhusu aondoke Simba aende Yanga, maana kulikuwa na matatizo, hata mama yake alisema ingawa yeye ni Simba, lakini aachwe mwanaye atoke kutokana na hali iliyokuwepo.
“Aliwahi kupigwa na kipa wao lakini viongozi hawakuchukua hatua yoyote hivyo, tuliona anaweza kupata matatizo makubwa zaidi acha aondoke, maana hakikuwa kitendo cha kiungwana.
“Kuongeza mkataba mpya Yanga ilishindikana sababu ya pesa aliyokuwa anahitaji, Kessy anatafuta maisha na hiyo ndiyo kazi yake, asingepata timu nje basi kwa hapa kama Yanga ingeshindikana ilikuwa ni kurudi tu Mtibwa Sugar ila alipopata Nkana tulimpa baraka zote kwenda kutafuta maisha,” anaeleza.
BIBI REHEMA ANATAKA ZAWADI
Ni bibi wa makamo, hata alipokuwa akizungumza na Mwanaspoti aliweka wazi kuwa taarifa zote za Kessy zinapatikana kwa bibi yake mdogo, ambaye ni Moshi Mohamed Kingunde ila alisema mambo machache tu juu ya mjukuu huku akisisitiza kutohitaji kulisikia jina la baba yake Hassan Kessy.
“Mwambieni Hassan awe ananikumbuka huko aliko, ni mjukuu na mtoto wangu, nampenda sana, Kessy hana matatizo yoyote ni kijana mwema tumemlea hapa hapa, alikuwa anakaa humu ndani na baadhi ya mizigo yake ipo humu, hapa ni kwake.
“Namuombea tu apate baraka nyingi, afanikiwe na kwa vile anatambua cha kufanya basi anajua atatufanyia nini kupitia mafanikio yake ya mpira, kama sio leo basi hata kesho, kikubwa Mungu ampe uzima na afya njema,” anasema Bibi Kessy anayejulikana kwa jina la Rehema Kessy.
LIKIZO YAKE MORO NI KULALA TU
Ndugu zake wanaweka wazi kwamba, kikubwa ambacho Kessy anapenda kukifanya akienda kwao Morogoro ni kutembelea ndugu na rafiki zake ila shughuli za nyumbani sio sana kuzifanya.
“Unajua muda mwingi anakuwa bize na kazi yake, hivyo akija huku kwenye mapumziko basi muda wake anautumia kulala, kutembelea wenzake, shughuli zingine hapana,” anasema.
MAISHA YA NDOA
Bibi Moshi anaweza wazi uhusiano na Kessy na nyota wa soka la wanawake nchini, Asha Mwalala, kuwa ndiye mchumba wake waliotambulishwa na wanamtambua huyo, wametoa baraka zote endapo atafikia maamuzi ya kufunga naye ndoa.
“Ninamfahamu mmoja tu Asha, ambaye hata hapa huwa anakuja ingawa hajafunga naye ndoa, tumetambulishwa rasmi hata kipindi kile alipokuwa na matatizo na Simba alikuja naye hapa kwa ajili ya mapumziko, ni huyo tu tunayemfahamu.
“Kessy hawezi kuchaguliwa mke, anapaswa achague mwenyewe kwani ndiye atakayeishi naye, sisi kazi yetu ni kumpa baraka kama alivyotutambulisha Asha Mwalala tuliwapa baraka zetu,” anasema
BABA NAYE AFUNGUKA
Wakati upande wa mama ukidai kwamba baba mzazi wa Kessy ni kama hakumpa ushirikiano mwanaye tangu walipotengana na mama yake, baba wa Hassan Kessy mzee Ramadhani maarufu kama Kidingile anafafanua.
“Katika familia kuna mambo mengi yanatokea, mazuri na mabaya, yote tunapaswa kuyapokea kwani ni mpango ya Mungu na huwezi kujua kwanini Mungu anakupangia upitie changamoto hizo.
“Sio kweli kwamba sijamsaidia Kessy katika maisha yake ya kawaida na ya mpira, mimi kama baba nimeshiriki vyote ingawa kuna changamoto za hapa na pale zilijitokeza na zinajitokeza na huenda zitaendelea kujitokeza maana haya ndiyo maisha yetu binadamu.
“Kessy ana mdogo wake ambaye wote wamezaliwa kwa mama mmoja kwa maana ya kwamba ni watoto wangu mimi, nilitengana na mama yao na Kessy amelelewa hapa kwa baba yangu ambaye ni babu yake yeye.
“Ameishi kwangu hadi darasa la tatu, nilimpeleka shule na kumfuata na aliamua kuacha shule akiwa darasa la tatu, alinieleza ukweli kuwa anataka shule ambayo atacheza mpira, alipelekwa Bagamoyo kwa Idd Kipingu, lakini baadaye kuna mpango ulifanywa wa kwenda kwenye kituo cha TFF walikuja watu kutoka Bolton Wonderers ya England.
“Ilibidi atoroke darasani na kuacha begi ili apate hayo mafunzo kwa hao wazungu na baadaye alikwenda kituo cha Manchester City cha Ghana ambako alifanya vizuri na kukubalika na hapo ndipo alipoitwa timu ya taifa ya vijana na kwa mara ya kwanza alicheza mechi dhidi ya Botswana.
“Hivyo masomo yake aliyaacha moja kwa moja akiwa kidato cha kwanza kwa Kipingu ambako alikwenda kusoma baada ya huku Morogoro kugoma kuwa anataka shule ya michezo,” anasema baba mzazi huyo wa Hassan Kessy.
SIRI YA JINA
Kessy ni jina la ukoo upande wa mama yake mzazi, kwake yeye anaitwa Hassan Hamis Ramadhan mjukuu wa Cheka Kiangile Mtwagwa ‘Kidingile’ ambaye ni babu yake na Mzee Ramadhan.
Mzee Ramadhan anasema hafurahishwi na mwanaye alivyoanza kujiita Kessy, jina linalotambulika zaidi kwa sasa.
“Nilimwita na kumweleza kutumia jina hilo ni kunibadilisha, ndipo nikamwambia aende TFF akabadilishe atumie majina yanayotambulika katika vyeti vyake ambayo ni majina.
“Kweli alikiri kuwa hajafanya vyema, na hilo Kidingile analojiita ni la upande wangu, wakati nacheza kuna mchezaji badala ya kuniita Kiangile alikuwa anatamka Kidingile ndipo lilizoeleka hivyo,” anasema.