Hamdi aingiwa ubaridi fainali FA kisa kikosi cha Singida BS

Muktasari:
- Hata hivyo, kocha huyo amesema anapambana na hali hiyo kwani hana namna ya kufanya zaidi ya kuzicheza mechi hizo na kufanikisha malengo.
KUCHEZA mechi nne za mashindano ndani ya kipindi cha takribani siku 11, imeonekana kuwa ni changamoto kwa Kocha Mkuu wa Yanga, Miloud Hamdi.
Hata hivyo, kocha huyo amesema anapambana na hali hiyo kwani hana namna ya kufanya zaidi ya kuzicheza mechi hizo na kufanikisha malengo.
Hamdi ameyasema hayo Yanga ikijiandaa na mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Singida Black Stars utakaochezwa kesho Jumapili Juni 29, 2025 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Mechi hiyo iliyopangwa kuanza saa 2:15 usiku, utahitimisha rasmi msimu kwa timu hizo ambapo Yanga inahitaji kutetea ubingwa iliouchukua msimu uliopita ikiifunga Azam kwa penalti 6-5 uwanjani hapo.
Akizungumzia mchezo huo, Hamdi ameanza kwa kuipongeza Singida kufuzu fainali, huku akibainisha hakushangazwa kuona timu hiyo ikifunga Simba nusu fainali.
"Kwanza nawapongeza Singida Black Stars kufuzu fainali, sikushangazwa na hilo, nilitegemea watakuwa na matokeo mazuri kwa sababu wamebadilisha mambo mengi sana, wakijijenga kuwa klabu kubwa, naamini watafanikiwa kwa hilo," amesema Hamdi na kuongeza;
"Singida ni timu nzuri, wameshinda nusu fainali dhidi ya Simba, sikushangazwa na hilo, Hii mechi ni muhimu kila upande."
Kocha huyo aliyeiongoza Yanga kutetea taji la Ligi Kuu Bara kwa kuifunga Simba 2-0 katika mechi ya kufungia msimu ameongeza kwa kusema; "Kwa upande wetu huu ni mchezo wa nne ndani ya siku 10, ni ngumu kwetu lakini lazima tucheze.
"Kesho tunafahamu mchezo utakuwa mgumu kwa sababu Singida wana timu nzuri, wana wachezaji wazuri na wamekuja kushinda kama ilivyo kwetu. Utakuwa mchezo mzuri ukizikutanisha timu nzuri."
Yanga inaenda kukabiliana na Singida ikiwa ni mechi ya nne kucheza ndani ya siku 11.
Juni 18, 2025, Yanga iliifunga Tanzania Prisons mabao 5-0 kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, kisha Juni 22, 2025 ikaishushia Dodoma Jiji kipigo kama hicho kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar. Juni 25, 2025, ikaichapa Simba 2-0 kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar. Hizo zote zilikuwa mechi za Ligi Kuu Bara. Kesho Juni 29, 2025 itakuwa zamu ya kukabiliana na Singida Black Stars.
"Unapokuwa katika klabu kubwa kama Yanga ambayo viongozi wamefanya kazi nzuri ya kuleta wachezaji wengi wazuri, kazi yangu ni kufanya mabadiliko ya hao wachezaji, mechi tatu za nyuma nimefanya hivyo," amesema Hamdi namna anavyopambana kulinda ubora wa kikosi hicho na kukabiliana na mechi mfululizo.
"Najali sana kuhusu wachezaji wangu. Kila mmoja nampa nafasi ya kucheza, hapa tunaye Sheikhan na wengine ambao wamekuwa wakipata nafasi.
"Sitaki kuona nawaharibu wachezaji wangu kwa kuwaweka sana benchi au jukwaani, nafanya yanayowezekana kupata nafasi ya kucheza ili wawe tayari kufikia malengo tuliyonayo ya kushinda makombe," amesema Hamdi.
Kocha huyo amefichua kuwa, katika fainali ya kesho ambayo amekiri inazikutanisha timu mbili bora, anaamini kuna mstari mwembamba utakaomtenganisha bingwa.
"Kuna jambo dogo ambalo litatenganisha matokeo ambalo kila mmoja analihitaji kuweka tofauti. Inahitajika kazi ya ziada kufanikisha, kwa upande wangu nitafanya juhudi zote kushinda mchezo huu," amesema Hamdi.
Yanga ambayo ni watetezi wa Kombe la FA, itaikabili Singida katika fainali ya tano mfululizo, ambapo nne ilizocheza tangu 2020 hadi hiyo kesho, imeshinda tatu na kupoteza moja.
Ilipoteza kwa Simba kwa bao 1-0 mjini Kigoma msimu wa 2020-2021, kisha kushinda zilizofuata 2021-2022 ilipoilaza Coastal Union jiji Arusha, ikailaza Azam kwa bao 1-0 jijini Tanga katika fainali za 2022-2023 na msimu uliopita ikailaza tena Azam kwa penalti visiwani hapo.
Je, kesho itaibuka na ushindi au ikazuiwa na Singida inayosaka taji la kwanza la michuano hiyo? Tusubiri tuone!