Haji Mnoga : Mpemba anayetikisa kinoma huko England

Muktasari:
- Katika mchezo huo, Mnoga alivalia jezi yenye namba 36 mgongoni na alipata nafasi ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza ambapo alipangwa na kocha wa timu hiyo, Kenny Jackett kama beki wa kulia.
MIONGONI mwa klabu za England zenye utamaduni wa kuwatumia wachezaji wa Kiafrika ni Portsmouth ‘Pompey’, ambao ukirejea nyuma waliwahi kuwa na Sulley Muntari, Nwankwo Kanu na hata Kevin-Prince Boateng kabla ya sasa ambapo wanamtanzania, Haji Mnoga.
Mnoga ni chipukizi wa Kitanzania ambaye amekuwa na maendeleo mazuri kwenye klabu hiyo kiasi cha kuanza kupata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha Pompey ambayo ipo Ligi Daraja la Pili England ‘League One’.
Kinda huyo mwenye uwezo wa kucheza beki wa kati na kulia ni mzaliwa wa Portsmouth, ambaye baba yake ni Mtanzania lakini upande wa Mama yake ni Mwingereza.
Baba wa mchezaji huyo, ni mwanasoka ambaye aliwahi kukichezea kikosi cha vijana cha timu ya taifa ya Zanzibar chini ya miaka 17 kabla ya kuachana na soka na kujikita kwenye shughuli nyingine.
Baada ya kuzaliwa Mnoga, April 16, 2002, alianza kupata elimu ya msingi kwenye shule ya Trafalgar katika mji wa Portsmouth.
Maisha yaliendelea kwa nyota huyo wa Kitanzania kama ilivyo kwa wanasoka wengine ambao wapo kwenye mataifa yaliyoendelea akapata nafasi ya kujiunga na kituo cha soka cha Portsmouth, 2008.
Mnoga alilelewa hapo kwenye ngazi tofauti za soka la vijana na hatimaye Oktoba 9, 2018 akapata nafasi kwa mara ya kwanza akiwa na miaka 16 ya kukichezea kikosi cha kwanza cha Portsmouth kwenye mchezo wa Kombe la EFL dhidi ya Crawley Town F.C.
Katika mchezo huo, Mnoga alivalia jezi yenye namba 36 mgongoni na alipata nafasi ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza ambapo alipangwa na kocha wa timu hiyo, Kenny Jackett kama beki wa kulia.
Beki huyo alicheza kwa dakika 65 ambazo zilitosha kuisaidia Portsmouth kuibuka na ushindi mwembamba kwenye mchezo huo wa bao 1-0, nafasi yake kuchukuliwa na Tom Naylor.
Baada ya mchezo huo kumalizika, beki huyo alisema anashukuru kocha wake kwa kumuamini pamoja na udogo wake wa umri na kuamua kumpa nafasi ambayo anadai ilimpa uzoefu mpya kwenye soka lake.
“Nimejisikia furaha, kucheza mchezo wangu wa kwanza, hakika nimepata uzoefu mpya, asante kwa yeyote ambaye amehusika katika safari yangu ya soka hadi kufika hapa nilipo.
“Huu ni muda wa kupambana ili kuendelea kupiga hatua zaidi, natambua kuwa nitakabiliwa na changamoto nyingine ambazo ni kubwa zaidi ya zile nilizokua nikikutana nazo kwa vijana,” alisema Mnoga. Huo ulikuwa mwanzo wa Mnoga kuanza kuaminika na taratibu kupata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha Kocha Kenny Jackett na hivi karibuni alipewa tena nafasi ya kucheza kwenye robo fainali ya kombe la EFL.
Portsmouth imetinga nusu fainali ya kombe hilo, baada ya kuifunga Peterborough United bao 1-0, Januari 22 huku Mnoga akicheza kwa dakika 56.
Katika hatua ya nusu fainali Portsmouth itakutana na Bury, Februari 26 huku mchezo wa nusu fainali ya pili ukiwa kati ya Bristol Rovers na Sunderland.
Kuna kila dalili za Mnoga kuendelea kupata nafasi ya kucheza kwenye mchezo huo wa nusu fainali kutokana na kocha wa timu hiyo, kutumia wachezaji wake muhimu kwenye michezo ya Ligi Daraja la Pili ili wapate nafasi ya msimu ujao kushiriki ‘Championship’.
Portsmouth upande wa Ligi Daraja la Pili ipo nafasi ya pili nyuma ya Luton Town ikiwa na pointi 57 ambazo wamezivuna katika michezo.
Mnoga ndiye mchezaji pekee wa Kitanzania ambaye yupo kwenye timu ya daraja la juu zaidi England, Mbongo mwingine anayecheza soka la kulipwa nchini humo ni Adi Yussuf wa Solihull Moors F.C. ya Ligi Daraja la Nne.
Beki huyo anaweza kufuata nyazo za mastaa kibao wa Kiafrika mabao walipita kwenye klabu hiyo na kufanya makubwa kwenye klabu nyingine mfano hai ni Boateng ambaye aliichezea AC Milan na sasa ametua FC Barcelona.