GSM rasmi Yanga
MFADHILI wa klabu ya Yanga, Ghalib Mohamed amewaongoza wanachama wa klabu hiyo kuanza kupokea kadi zao mpya za utambulisho wa wanachama huku naye akiwa mwanachama rasmi.
Ghalib alipokea kadi yake jana ofisini kwake jijini Dar es Salaam hatua ambayo ilikuwa sambamba na wanachama wengine ambao walianza kuchukua kadi zao kupitia viongozi wao wa matawi makao makuu ya klabu ya Yanga.
Akizungumza jana, Ghalib alisema amefarijika kupokea kadi yake ya utambulisho wa wanachama huku akisifia kuona ubora wa kadi hizo ambazo zitakuwa na heshima kwa wanachama wenzake.
Ghalib aliwapongeza uongozi wa Yanga na kampuni ya Kilinet ambao ndio wanaosimamia mchakato huo wa usajili wa kielektroniki akisema umekuwa ukiendelea kwa kasi na mafanikio makubwa.
“Nimefarijika sana kupokea kadi yangu hii imekuwa ni ndoto kwangu na kampuni yetu ya GSM lakini pia uongozi wa Yanga, hizi kadi zina ubora mkubwa na niwaombe wanachama wenzangu ambao bado hawajajisajili wafanye hivyo haraka kwa maslahi ya klabu yetu,” alisema Ghalib.