Goran aomba mechi mbili za kutesti

Muktasari:
- Pamba Jiji ilirejea jijini hapa mwishoni mwa wiki iliyopita ikitokea Morogoro ilikokuwa imeweka kambi ya wiki mbili na imeanza kujifua jijini Mwanza kumalizia maandalizi yake ya wiki tano kwa msimu mpya.
WAKATI maandalizi ya Pamba Day yakizidi kunoga, Kocha wa Pamba Jiji, Goran Kopunovic ameomba mechi mbili kutesti mitambo ya kikosi chake baada ya kujifua kwa wiki nne mjini Morogoro na Mwanza.
Pamba Jiji ilirejea jijini hapa mwishoni mwa wiki iliyopita ikitokea Morogoro ilikokuwa imeweka kambi ya wiki mbili na imeanza kujifua jijini Mwanza kumalizia maandalizi yake ya wiki tano kwa msimu mpya.
Meneja wa timu hiyo, Ezekiel Ntibikeha alisema kocha huyo ameomba mechi mbili kupima kikosi chake ili kuona kama kimeanza kuiva na kupata muunganiko na mchezo wa kwanza utapigwa kesho kwenye Uwanja wa Nyamagana na timu mojawapo kutoka Kanda ya Ziwa.
“Maandalizi yetu ni ya wiki tano na tulifanya wiki mbili hapa Mwanza na mbili Morogoro, tumerudi Mwanza tunaendelea na maandalizi na baada ya kufika hapa mwalimu ameomba mechi mbili za kirafiki, tunaendelea kufanya mawasiliano na timu,” alisema Ntibikeha na kuongeza;
“Tutakuwa na mchezo Jumamosi Nyamagana na kabla ya siku ya Pamba (Pamba Day) tutakuwa na mchezo mwingine, ukanda wetu huu timu nyingi ni za Championship bado hazijaanza maandalizi, tunatafuta timu ambayo iko tayari.”
Timu hiyo itacheza na Vital’O ya Burundi katika kilele cha tamasha lake Agosti 10, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza ambalo litanogeshwa na burudani za wasanii, huku akidokeza jezi mpya za timu hiyo zitakuwa tayari kabla ya tamasha ili mashabiki wazivae siku husika.
Mwenyekiti wa hamasa Pamba Day, Amina Makilagi alisema tamasha hilo litaacha alama kwani wamejiandaa kufanya mambo makubwa, huku Ofisa habari Makilagi – tumejiandaa kufanya vizuri tunataka tuache alama kwenye tamasha hili
Ofisa Habari wa klabu hiyo, Martin Sawema alisema; “Sisi kwa sababu ni wakubwa tumeamua kujipima na wakubwa wenzetu, tunawaomba wapenzi wa soka waendelee kukata tiketi kwa wawakilishi wetu walioko maeneo mbalimbali ya mkoa wetu.”