Gomez wa Fountan Gate auanza mwaka vibaya

Muktasari:
- Nyota huyo mwenye mabao sita ya Ligi Kuu Bara sawa na Clement Mzize wa Yanga, akipitwa na Elvis Rupia wa Singida Black Stars aliyefunga manane na Jean Charles Ahoua wa Simba mwenye saba, amejitonesha tena mazoezini na kushindwa kucheza na Yanga.
MSHAMBULIAJI wa Fountain Gate, Seleman Mwalimu ‘Gomez’ ameendelea kukumbwa na majanga baada ya kuumia tena nyama za paja, ambazo zilimfanya kukosa mchezo wa timu hiyo dhidi ya Yanga, ambao kikosi hicho kilichapwa mabao 5-0, Desemba 29, mwaka jana.
Nyota huyo mwenye mabao sita ya Ligi Kuu Bara sawa na Clement Mzize wa Yanga, akipitwa na Elvis Rupia wa Singida Black Stars aliyefunga manane na Jean Charles Ahoua wa Simba mwenye saba, amejitonesha tena mazoezini na kushindwa kucheza na Yanga.
Mshambuliaji huyo alikosa mchezo wa Kombe la Shirikisho hatua ya 64, dhidi ya Mweta Sports ya Mwanza ambao Fountain Gate ilishinda kwa mabao 2-0, kisha akakosa tena wa Ligi Kuu Bara mbele ya Coastal Union walioshinda 3-2, Desemba 13, jana.
Baada ya hapo akaibuka dhidi ya Azam FC Desemba 17, mwaka jana ambao timu hiyo ilichapwa mabao 2-0, ingawa baada ya hapo hakucheza tena mchezo uliopita na Yanga, kutokana na kuumia nyama za paja akiwa mazoezini na kikosi hicho cha Manyara.
“Nilipata changamoto hizo na kwa bahati mbaya nikashindwa kucheza mchezo wetu uliopita na Yanga, kiukweli inaniuma sana kama mchezaji kwa sababu shauku yangu kubwa ni kuona nazidi kupambana na kuisaidia timu yetu ifanye vizuri,” alisema na kuongeza anaendelea vyema na programu maalumu.