Gomes amaliza kazi, Morrison kuikosa Kagera Sugar

Muktasari:

Simba ikiwa mikoa ya kanda ya ziwa itacheza mechi tatu ambapo tayari imeshaanza kazi kwa kuwalaza Mwadui na kesho watakuwa mjini Bukoba kukipiga na Kagera Sugar.

Mwanza. Wakati Simba ikijiandaa kwa ajili ya mchezo wao wa kesho dhidi ya Kagera Sugar, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Didier Gomes amesema nyota wake wako fiti kwa mapambano huku akimtaja Bernard Morrison kukosa mechi hiyo.

Simba baada ya mchezo wao uliopita dhidi ya Mwadui walioshinda bao 1-0 huko mjini Shinyanga juzi Jumapili, walirudi jijini Mwanza na jana jioni walijifua katika uwanja wa Nyamagana.

Licha ya mazoezi hayo kukosekana kwa baadhi ya wachezaji wanaounda kikosi cha kwanza, lakini Gomes na wasaidizi wake katika benchi la ufundi walionekana kuwa makini kutengeneza vitu mbalimbali kwa nyota wao kama kufunga mabao, kupiga pasi, kukaba, kumiliki mpira na kupiga vyenga.

Akizungumza baada ya mazoezi hayo, Gomes alisema mechi iliyopita alibaini baadhi ya makosa kwa wachezaji wake haswa kwa kushindwa kufunga mabao jambo ambalo amelifanyia kazi.

Amesema anaamini mchezo wa kesho vijana wake watafanya vizuri licha ya kwamba anafahamu ushindani utakuwapo katika mechi hiyo kutokana na hali ya wapinzani wao.

"Morrison ndiye atakosa mechi hiyo kwa sababu ya kuwa na kadi tatu za njano lakini wengine wote wako vizuri na hawa ambao hawapo kwenye mazoezi wamepumzika kwa sababu jana (juzi) walicheza dakika 90" amesema Gomes.

Hata hivyo Kocha huyo amefafanua kuwa moja ya mikakati yao ya kufikia malengo ya kushika usukani ni kupambana kila mechi kupata alama tatu na kwamba kutocheza kwa baadhi ya wachezaji si kwamba wana matatizo yoyote.

"Hao ambao hawajacheza si kwamba wana matatizo au siwaamini, kila mtu ana umuhimu wake kikosini na anatumika kulingana na mchezo husika ndio maana leo (jana) unaona mazoezini wapo hivyo anayeonesha uwezo namtumia" amesema Mfaransa huyo.