Giniki hayupo kambini, sababu ni hii

SHIRIKISHO la Riadha nchini (RT) limetoa sababu za kwa nini mwanariadha, Emmanuel Giniki hayuko katika kambi ya Taifa inayojiandaa na michuano ya Jumuiya ya Madola.
Kambi hiyo yenye jumla ya wanariadha 15, inayonolewa na kocha mwandamizi wa riadha nchini, Sulemani Nyambui, iko katika hosteli za chuo Cha misitu eneo la West Kilimanjaro Wilaya ya Hai.
“Andrew Rhobi ni mkimbiaji wa Mbio za Mita 800 moja ya tukio iliyopo kwenye michezo ya jumuiya ya madola hivyo lazima awepo kambini, lakini Giniki anakimbia na kufanya vizuri sana kwenye mbio za Kilometa 21,haipo kule sasa tufanyeje hapo,” alisema Katibu Mkuu wa RT, Jackson Ndaweka.
Ndaweka amejibu hivyo baada ya kuwepo kwa maswali mengi ya wadau wanaohoji uhalali wa mwanariadha Rhobi kuwa miongoni wachezaji waliochaguliwa kuunda timu ya Taifa huku akikosekana Giniki anayefanya vizuri katika mashindano ya kimataifa ikiwemo Kilimanjaro Marathon na Warsaw marathon huko Poland .
Ndaweka alisema katika kuchagua timu ya taifa mambo mengi wamezingatia ikiwamo malengo ya mchezaji mwenyewe na hakuna aliyependelewa bali kila anayefanya vizuri atashiriki mashindano ya Taifa.
“Muwape muda na kuwaunga mkono kwani ni Watanzania wenzetu na iwapo watafanya vizuri basi sifa itarudi kwetu sote, tusiwabague na kuwakatisha tamaa, zaidi muda utaongea, tutaona kama maamuzi yalikuwa sahihi au vinginevyo,” alisema Ndaweka.
Kwa upande wake kocha mkuu wa timu hiyo ya taifa, Seleman Nyambui alisema wachezaji wote waliopo kambini wana sifa ya kuwepo hapo hivyo kuomba asiingiliwe.