Gia ya MO yamzidi maarifa Manji

Muktasari:
Kwanza, Simba imeweka posho kubwa kwa wachezaji wao ambayo ni zaidi ya mara mbili ya waliyokuwa wakipewa wachezaji wa Yanga wakati wanashinda mataji matatu msimu uliopita. Wachezaji wa Yanga walikuwa wakipewa posho ya Sh 70,000 kwa mechi wanazoshinda huku uongozi ukiongeza pindi ulipoona inafaa.
SIMBA haiko vizuri kiuchumi kama watani zao Yanga, lakini imejidhatiti katika maeneo kadhaa ambayo yameanza kuwaweka Yanga tumbo joto hasa bosi wao Yusuf Manji ambaye amekuwa akidai kuwa Simba haiwezi kutamba wakati akiwa bosi wa timu hiyo.
Kwanza, Simba imeweka posho kubwa kwa wachezaji wao ambayo ni zaidi ya mara mbili ya waliyokuwa wakipewa wachezaji wa Yanga wakati wanashinda mataji matatu msimu uliopita. Wachezaji wa Yanga walikuwa wakipewa posho ya Sh 70,000 kwa mechi wanazoshinda huku uongozi ukiongeza pindi ulipoona inafaa.
Simba kwa sasa inatoa posho ya Sh 10 milioni kwa kila mechi ambayo wanashinda na kuwagawanyia wachezaji ambapo katika kiwango hicho bilionea Mohammed Dewji anachangia Sh 5 milioni huku mabosi wengine wa timu hiyo wakitoa kiasi kama hicho pia. Kila mchezaji wa Simba amekuwa akiondoka na zaidi ya Sh 200,000 kama posho katika kila mechi wanayoshinda.
Pili, Simba imeanza kutumia usafiri wa anga katika mechi zao za mikoani ambapo imekuwa ikipata fedha za kugharamia usafiri huo kutokana na michango ya wadau wa timu hiyo ambao wamekuwa wakinunua tiketi na kuwapatia viongozi. Awali, Yanga na Azam pekee ndizo zilizokuwa zikitumia usafiri wa anga katika mechi za mikoani.
“Hapo kwenye posho hakuna longolongo, tulianzisha huo utaratibu katika mechi ya JKT Ruvu ambapo milioni 10 ziliwekwa mezani lakini tukapata sare, tukasema labda imekuwa presha kubwa kwa wachezaji lakini sasa tunaona utaratibu huo unakwenda vizuri,” alisema kigogo mmoja wa Simba na kudai kuwa ikitokea mtu amejitolea fedha zaidi wamekuwa wakiwapa pia wachezaji. Akizungumzia mambo ya ndani ya uwanja ambayo yanawabeba msimu huu, nahodha wa zamani wa Simba, Mussa Hassan Mgosi alisema kocha amekuwa akifanya mzunguko kwa wachezaji wake jambo ambalo limeongeza kiu ya kujituma kwa kila mmoja.
“Unajua hapa kila mmoja ana nafasi ya kucheza, kocha ameamua hakuna staa, na tunaona kila mmoja anafanya kazi kwaajili ya timu, ni jambo jema kwetu sote,” alisema Mgosi ambaye ni meneja wa timu hiyo.
MABAO YA USIKU YAIPONZA
Simba ilipoteza mchezo wake wa kwanza juzi Jumapili dhidi ya African Lyon ya Dar es Salaam lakini imebainika kuwa tabia ya timu hiyo kutegemea mabao ya usiku imeiponza.
Tathmini ya msimu huu inaonyesha kuwa Simba kwa kiwango kikubwa imekuwa ikipata matokeo ya ushindi katika kipindi cha pili jambo ambalo juzi liliwagomea na kujikuta wakifungwa bao la usiku na Lyon hivyo kuvunja rekodi yake hiyo iliyotukuka.
Msimu huu, Simba imefunga mabao 25 lakini ni mabao manne tu ambayo imefunga katika dakika 20 za mwanzo jambo ambalo limekuwa likiwaweka katika wakati mgumu wa kupata ushindi katika baadhi ya mechi.
Simba ilifunga bao la mapema zaidi katika mechi ya Majimaji ambapo Jamal Mnyate alifunga katika dakika ya nne tu. Mechi nyingine Simba ilifunga bao la mapema dhidi ya Mbeya City ambapo Ibrahim Ajibu alifunga katika dakika ya 6 na dhidi ya Ruvu Shooting ambapo alifunga katika dakika ya 11. Mavugo alifunga katika dakika ya 20 kwenye mchezo na Ndanda.
Rekodi zinaonyesha kuwa kati ya mabao 25 ya Simba msimu huu, timu hiyo imefunga mabao 15 katika kipindi cha pili jambo ambalo limekuwa likiwaweka roho juu mashabiki wa timu hiyo.
Mabao ya usiku zaidi ya Simba ni dhidi ya Yanga na Mbao FC ambapo yalifungwa katika dakika ya 86 na Shiza Kichuya pamoja na Mzamiru Yassin.