Fiston apewa mifumo mitatu Yanga

KOCHA wa Yanga, Cedrick Kaze amesisitiza kwamba anayaamini makali ya straika mpya aliyemsajili kwenye dirisha dogo, Fiston Abdul Razak. Lakini Makamu Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Yanga, Hersi Said ametamka kwamba mziki wao wanaoingia nao sasa umetimia ; “yeyote tunayekutana nae atapigwa tu, tusilaumiane.” Yanga pia imesajili beki wa kati, Dickson Job kutokea Mtibwa Sugar na Said Ntibazonkiza wa Burundi.

Usajili wa Job katika kikosi cha Yanga una maana kwamba anakwenda kuwa mbadala wa mabeki wa kati Lamine Moro na Bakari Nondo Mwamnyeto waliotumika mara kwa mara lakini anategemewa zaidi katika siku zijazo kutokana na umri wake.

Yanga wamefanya usajili wa Fiston kutokana na mastraika waliokuwepo katika kikosi hicho kwenye duru la kwanza hawakufanya vizuri kwani mpaka wanacheza michezo 18, vinara walikuwa Yacouba Songne na Michael Surpong ambaye kila mmoja alikuwa amefunga mabao manne.

Mwanaspoti imemfanyia tathimini staa huyo mpya wa Yanga, kulingana na ambavyo alikuwa akicheza katika klabu mbalimbali kama Mamelodi Sundowns, Rayon Sports, De Agosto na JS Kabylie anaweza kuingia katika kikosi cha kwanza na akacheza vizuri katika mifumo mitatu.

Mfumo wa kwanza aWmbao Fiston (4-4-2), hapa anaweza kucheza nyuma ya straika kwa maana ya watu wawili wa mbele anaweza kuwa pamoja na Yacouba au Sarpong wakati nyuma yao kulia atakuwepo Tuisila Kisinda, kushoto Saido Ntibazonkiza na viungo wawili wa kati Mukoko Tonombe na Feisal Salum.

Mfumo wa pili ambao Fiston anaingia katika kikosi cha kwanza kama atakuwa fiti (4-3-3), atacheza katika watu watatu wa mbele ambao wanaweza kuwa pamoja na Saido na Tuisila ambao watakuwa wanacheza kwa kupishana kushoto na kulia.

Nyuma yao kutakuwa na viungo wengine watatu, Mukoko, Fei Toto na Deus Kaseke ambao watakuwa na majukumu mawili kwanza kuhakikisha wanalikamata eneo la kiungo na viungo wa timu pinzani kutokusumbua pamoja na kupeleka mipira mingi kwa washambuliaji hao watatu wa mbele wenye uwezo wa kutengeneza nafasi za kufunga na kufunga wenyewe.

Fiston katika mfumo huu, atakuwa akicheza kwa kujiachia kwa maana jukumu lake la kwanza litakuwa kufunga kutokana na nafasi ambazo zitatengenezwa na viungo au washambuliaji wenzake Saido na Tuisila, lakini muda ambao atakuwa amebanwa nae atakuwa na jukumu la kutengeneza nafasi za kufunga kwa wenzake.

Shida ambayo Yanga wataipata katika mfumo huu uwepo wa Fiston, Tuisila na Saido katika safi yao ya ushambuliaji maana yake pindi wanapopoteza mpira hawa wote si wazuri katika kukaba na maana yake Kaseke, Fei Toto na Mukoko wanatakiwa kuwa imara na bora katika kukaba. Kutokana na uwezo wake mkubwa aliokuwa nao wa kumiliki mpira mguuni kwake, kupiga pasi zenye macho kwa walengwa, kufunga mwenyewe kwa kutumia miguu yake miwili pamoja na kichwa mfumo wa tatu ambao unaweza kumfaa (4-2-3-1).

Hapa anacheza katika nafasi mbili ya kwanza katika eneo la viungo watatu washambuliaji ambalo anaweza kuwa sambamba Tuisila na Kaseke ambao majukumu yao yatakuwa kutengeneza nafasi za kufunga kwa straika anaweza kuwa mmoja kati ya hawa, Sarpong, Yacouba, Waziri Junior au Ditram Nchimbi na muda mwingine kufunga wenyewe.

Katika mfumo huo eneo la pili ambalo anaweza kucheza ni straika na nyuma yake katika eneo la viungo watatu ataongezeka Saido ambaye atakuwa sambamba na Tuisila, Kaseke, Yocouba au mmoja kati ya hawa Haruna Niyonzima, Farid Mussa na Carlos Carlinhos.

Nyota hao sita ambao wanaweza kuwa katika wakati mgumu wa kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara kutokana na usajili wa Fiston ni Waziri, Carlinhos, Sarpong, Niyonzima, Farid na Ditram Nchimbi.

Sababu ambazo zinahatarisha nafasi ya kucheza mara kwa mara kwa wachezaji hao sita kwanza wanacheza nafasi moja na mchezaji huyo mpya, kabla ya usajili wa Fiston ukimuondoa Sarpong wengine wote walikuwa wakiishia benchi au kucheza muda mchache.

Wachezaji hao sita kablaya usajili wa Fiston katika kikosi cha Yanga wameonekana kushindwa kufanya vizuri na kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara.


MSIKIENI MWENYEWE

Fiston anasema; “Nina imani kuna kitu nitakiongeza katika timu yangu mpya haswa kwenye kufunga mabao jambo ambalo hata mimi mwenyewe nalipenda.”

“Yanga ni timu ya wananchi nitapambana ili kutimiza majukumu yangu ambayo yatawafanya wanchi wafurahi,” aliongeza Fiston.

Juzi kati, mtupiaji wa zamani wa Yanga, Amissi Tambwe alisema Fiston ni moja ya usajili bora wa Yanga kuwahi kutokea na anaweza kukaribia rekodi zake Jangwani.