Fei Toto ang'oka Yanga, sasa njia nyeupe Azam

Muktasari:

  • Fei kwa sasa amebakiza mkataba wa mwaka mmoja na nusu hadi 2024 kuitumikia Yanga na tayari mabosi wa klabu hiyo walikuwa wakijadili ombi lake la kutaka kuboreshewa mshahara kutoka Sh4 milioni anaolipwa sasa hadi kuwa Sh10 milioni, lakini mabosi wa Yanga ni kama wanasikilizia sana.

HUENDA isiwe taarifa nzuri kwa mashabiki wa Yanga, lakini ndivyo ilivyo inadaiwa kuwa, kiungo fundi wa timu hiyo, Feisal Salum ‘Fei Toto’ anajiandaa kuondoka klabuni hapo.
Kiungo huyo aliyesajiliwa misimu minne iliyopita kutoka JKU ya Zanzibar, inaelezwa ameamua kuvunja mkataba na klabu hiyo ili awe huru kujiunga na timu yoyote kupitia dirisha dogo la usajili lililopo wazi hadi Januari 15 mwakani.
Tangu mapema, Fei mwenye mabao sita katika Ligi Kuu Bara msimu huu na asisti mbili, amekuwa akihusishwa na klabu ya Azam, ila pande zote ikiwamo mchezaji mwenyewe, wamekuwa wakikanusha juu ya kuwepo kwa dili hilo.
Hata hivyo, chanzo cha kuaminika kilicho karibu na kiungo huyo kimesema, Fei ameamua kujichomoa klabuni hapo kutokana na kutotekelezwa kwa ishu yake ya kimasilahi ikiwamo ombi la ongezeko la mshahara anaolipwa Yanga.
Chanzo hicho makini kililithibitishia Mwanaspoti kuwa, Fei amewaeleza kuwa hana furaha klabuni hapo kutokana na kuona wachezaji kadhaa wa kigeni wakilipwa fedha nyingi, huku wakiwa wanaishia kukaa jukwaani tu na wengine wakiwa na mchango, ilihali yeye anayeipigania timu akilipwa fedha kiduchu na hasikilizwi kilio chake.
“Amekuwa akilalamika kila mara kuwa, ndani ya Yanga kuna wachezaji wanalipwa fedha nyingi na wamepangiwa kwenye nyumba za bei ghali, lakini hawaitumikii timu, jambo ambalo limekuwa likimshusha morali na kuhisi hathaminiwi, japo amekuwa akiuomba uongozi umboreshee masilahi, lakini umekuwa ukimpotezea,” kilisema chanzo hicho ambacho ni rafiki wa karibu wa Fei Toto, aliyeongeza; “Kwa sasa ameamua ni heri aachane nayo, ili aangalie mahali penye masilahi mazuri kwa maisha yake ya baadaye.”
Chanzo hicho kilichoombwa kuhifadhiwa jina, kilisema katika kuhakikisha anakuwa salama, Fei na jopo lake la wanasheria wameuchungulia mkataba alionao na Yanga na kubaini kipengele kinachomtaka kama atavunja mkataba ailipe klabu Sh100 milioni na mishahara ya miezi mitatu.
Ipo hivi. Fei kwa sasa amebakiza mkataba wa mwaka mmoja na nusu hadi 2024 kuitumikia Yanga na tayari mabosi wa klabu hiyo walikuwa wakijadili ombi lake la kutaka kuboreshewa mshahara kutoka Sh4 milioni anaolipwa sasa hadi kuwa Sh10 milioni, lakini mabosi wa Yanga ni kama wanasikilizia sana.
Lakini kuwepo kwa dili kadhaa kwa wanaomsimamia likiwemo la Azam na zile za kutoka nje ya nchi zilizoweka mezani mkwanja wa maana ikiwamo kumuahidi kumlipa zaidi ya mshahara anaotaka kulipwa na Yanga, mbali na fedha za usajili, nyumba yenye hadhi ya mchezaji wa kiwango chake na marupurupu mengine yamezidi kumdatisha Fei Toto.
“Kwa kweli Fei anataka kuondoka Yanga na jana alikuwa bize kuiingizia Yanga fedha kabla ya kutangaza kuvunja mkataba, ila sijui anaenda wapi,” kilisema chanzo hicho cha karibu cha Fei Toto.
Mmoja ya wachezaji wa Yanga ambaye ni rafiki wa karibu wa Fei (jina tunalo) naye alithibitisha kuwa, kiungo huyo alimdokeza juu ya dili la kuondoka akiitaja Azam huku akidai klabu hiyo imeweka fedha nyingi ambazo ni ngumu kwa mchezaji yeyote kuikataa.
Mchezaji huyo alisema nje na masharti ya Yanga, ofa ya Azam ya kutaka kumpa Fei pesa ya kusaini ya Sh390 milioni, mshahara wa Sh17 milioni kwa mwezi, nyumba ya kuishi ya Sh10 milioni na vitu mbalimbali, vimemchanganya mchezaji huyo baada ya kufahamishwa na mabosi wanaomsimamia.
Chanzo kingine cha karibu cha Fei kimethibitisha mchezaji huyo juzi aliingizia Yanga Sh100 milioni tayari kwa kuvunja mkataba na kwa mechi ya Jumapili ambayo Yanga itakuwa wageni wa Azam iko fifte fifte kucheza na huenda pia ikawa ndio mechi ya mwisho kwake kama mchezaji wa Yanga.
Alipotafutwa jana Fei na kuulizwa swali hilo alikata simu bila kujibu, huku Azam tangu mapema walianza kukanusha uvumi ulipoanza.