Prime
Fei Toto aingiza mabilionea vitani

Muktasari:
- Licha ya kuwa jamaa ana mkataba na Azam, lakini inadaiwa akili zake kwa sasa na kutaka kutua katika moja ya klabu kubwa hapa nchini, huku ikifichuka kwamba kuna bato kubwa imeibuka baina ya vigogo wa Simba na Yanga.
KIUNGO mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum 'Fei Toto' ameendelea kushika vichwa vya mashabiki wa soka kutokana na tetesi za kuanza kuwindwa na klabu kadhaa kwa ajili ya msimu ujao wa mashindano wa 2025-2026.
Licha ya kuwa jamaa ana mkataba na Azam, lakini inadaiwa akili zake kwa sasa na kutaka kutua katika moja ya klabu kubwa hapa nchini, huku ikifichuka kwamba kuna bato kubwa imeibuka baina ya vigogo wa Simba na Yanga.
Ndio kuna bato la maana linaendelea nje ya uwanja kati ya Simba na Yanga na safari hii sio kwa wachezaji au makocha bali ni matajiri wawili wa klabu hizo, wakichonganishwa na kiungo huyo anayeongoza kwa asisti 13 katika Ligi, huku msimu uliopita akimaliza wa pili kwa kufunga mabao 19.
Matajiri hao waliongia vitani ni bilionea Mohamed 'MO' Dewji anayepambana vikali na mwenzake wa Yanga, Ghalib Said Mohammed 'GSM' kila mmoja alipigana kivyake kuwania huduma ya kiungo huyo wa Azam FC ambaye inaelezwa amechomoa kuongeza mkataba mpya Chamazi ili asepe zake.
Fedha ambazo Fei Toto amewekewa na klabu hizo mbili ukiongeza na mvuto wa watani hao wa jadi ni vigumu kwa kiungo huyo kubaki ndani ya klabu yake ya Azam kwa msimu ujao.
Yanga mambo yapo hivi
Yanga kupitia GSM ndio wameweka fedha ndefu kwa Fei Toto kiasi cha Sh 800 Milioni ikitaka kumpa mkataba wa miaka miwili ofa yenye mshahara wa 40 Milioni.
Ofa hii ndio kubwa kuliko klabu zote mbili ukiondoa Azam zinazomtamani Fei Toto ambapo ndani yake pia kuna vitu vingine vya gharama.
MO na Simba yake
MO Dewji amekutana mara mbili na Fei Toto katika vikao vya siri, lakini ofa yake imebaki kuwa Sh 750 Milioni, ila mshahara umeongezeka kutoka Milioni 35 za awali kwa mwezi hadi 48 Milioni pia wakamjaribu kwamba akubali kusaini mkataba wa miaka mitatu.
Sharti hilo la muda wa mkataba ndio linaitingisha kambi ya Fei Toto ambapo bado wanaonyesha kushawishika na ofa ya Yanga.
Azam jeuri, lakini dah!
Azam ndio wenye jeuri kubwa ya fedha Mwanaspoti linafahamu kwamba matajiri hao wamemuwekea kiasi Cha sh 900 Milioni na mshahara mkubwa wa 45 Milioni, lakini kiungo huyo hajaonyesha kuhitaji kusalia hapo akiona kama anachelewa kung'aa zaidi.
Fei Toto amekuwa na miaka mizuri ya namba ndani ya Azam akikosa kidogo kuwa mfungaji Bora msimu uliopita akizidiwa na Stephanie Aziz KI kwa tofauti na mabao mawili, yeye akimaliza na 19 na Aziz Ki akiwa na 21, lakini msimu huu akiwa kinara wa asisti 13, hata hivyo anaona kama matajiri hao wa Chamazi wanafifisha jina kutokana na ubora wa kikosi chao.
Aziz KI atumika
Yanga imeshafanya biashara ya kwanza kumuuza kiungo Stephanie Aziz KI aliyetambulishwa juzi usiku pale Wydad Athletic ya Morocco akiuzwa kwa fedha ya kufuru Sh 2 Bilioni.
Tajiri wa Yanga wanataka Fei Toto arudi nyumbani kwenda kuvaa viatu vya Aziz KI ambapo inaelezwa hata raia huyo wa Burkina Faso wakati anaongea na mabosi wa klabu yake aliwataka kutopoteza muda, wakamchukue kiungo huyo ili azibe nafasi yake.