Fainali ASFC yawazuia Feitoto, Job kujiunga U23

KOCHA mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania kwa vijana wasiozidi umri wa miaka 23 Kim Poulsen ameeleza kuwa alipanga kuwaita wachezaji wa Yanga, Feisal Salum na Dickson Job kikosini kwake lakini imeshindikana kutokana na nyota hao kuwa na ratiba ngumu.
Kim leo ameweka wazi majina ya wachezaji 20 ambao wataingia kambini Jumatatu kujiandaa na michuano ya ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) itakayofanyika mwezi huu nchini Ethiopia huku Feisal na Job wakikosekana kutokana na klabu yao kuwa na mchezo wa fainali ya kombe la Azam (ASFC) dhidi ya Simba utakaopigwa Julai 25 mkoani Kigoma.
Kocha huyo raia wa Denmark ameeleza hayo leo kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika makao makuu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Karume Dar es Salaam.
“Nilipanga kuwajumuisha Feisal na Job, lakini wanakabiliwa na mchezo wa fainali hivyo nimewaacha na nimechagua wengine ambao naamini wataiwakilisha nchi vyema,” amesema Kim.
Sambamba na hao kocha Kim alimhitaji kipa wa Mwadui Mussa Mbissa, kwenye kikosi chake lakini imeshindikana kutokana na kuchelewa kwa upatikanaji wa baadhi ya nyaraka zake za kusafiria ikiwemo ‘Visa’ hivyo kumuita Daniel Mgore wa Biashara United.
Wachezaji walioitwa ni makipa Metacha Mnata (Yanga), Mgore (Biashara Utd), na Wilbol Maseke (Azam Fc) huku mabeki ni Israel Mwenda, Lusajo Mwaikenda (KMC), Nickson Kibabage (Youssoufia fc), Paschal Msindo, Sospeter Israel (Azam) Abdulmajid Mangalo (Biashara Utd) Abdulrazack Hamza (Mbeya City) na Oscar Masai wa Ihefu.
Viungo ni Lucas Lucas Kikoti (Namungo), Joseph Mkele (Mtibwa Sugar),Rajabu Athuman, Meshack Abraham
(Gwambina).
Washambuliaji ni Erick Mwijage, Yusuph Mhilu (Kagera Sugar), Reliant Lusajo (Namungo), Andrew Semchimba (Ihefu) na Abdul Seleman ‘Sopu’ (Coastal Union).
Reliant Lusajo, Mhilu na Sospeter (Bryson) ni wachezaji wa tatu waliozidi umri wa miaka 23 lakini wameitwa kwenye kikosi hicho kwa mujibu wa sheria inayoruhusu wachezaji watatu waliozidi umri kutumika kuongeza nguvu kikosini katika michuano hiyo ambayo Tanzania imepangwa kucheza na Congo DR na Uganda.