Prime
Fadlu ana kazi kubwa ya kufanya

Muktasari:
- Fadlu amesema kucheza na Waarabu hao nyumbani kwao inapaswa kufanyika nguvu ya ziada kuhakikisha timu haipotezi mchezo, hivyo kuwaweka sawa kisaikolojia wachezaji wake ndiyo mbinu mojawapo ya kufanikiwa.
WAKATI Simba ikitarajiwa kucheza dhidi ya CS Constantine ugenini, kocha mkuu wa kikosi hicho, Fadlu Davids amesema mbali na kufanya mazoezi, ana jambo la kufanya.
Fadlu amesema kucheza na Waarabu hao nyumbani kwao inapaswa kufanyika nguvu ya ziada kuhakikisha timu haipotezi mchezo, hivyo kuwaweka sawa kisaikolojia wachezaji wake ndiyo mbinu mojawapo ya kufanikiwa.
Mchezo huo wa pili wa Kundi A katika Kombe la Shirikisho Afrika, unatarajiwa kuchezwa Desemba 8 mwaka huu saa 1 usiku kwenye Uwanja wa Mohamed Hamlaoui uliopo katika Mji wa Constantine nchini Algeria.
Akizungumza na Mwanaspoti, Fadlu alisema kazi kubwa aliyonayo kwa sasa ni kuhakikisha anawajenga zaidi wachezaji wake kisaikolojia. “Kutocheza vizuri katika mchezo wa kwanza hasa kipindi cha pili ilikuwa ni presha ya kutafuta ushindi nyumbani, lakini tuna kikosi chenye wachezaji wengi vijana ambacho kimemeba malengo makubwa.
“Najua namna ya kucheza na saikolojia ya wachezaji wangu na watabadilika kuelekea mechi ijayo kwani mechi hizi zinawasaidia wapya kukomaa na ushindi tulioupata utawajenga kuelekea mechi ya ugenini, lakini nafahamu namna ya kuzicheza mechi za timu za Kaskazini mwa Afrika,” alisema.
Hii itakuwa ni mara ya pili msimu huu Fadlu anakwenda Ukanda wa Kaskazini mwa Afrika kucheza mechi ya Kombe la Shirikisho baada ya hatua ya mtoano kupambana na Al Ahli Tripoli ya Libya.
Katika mchezo wa kwanza nchini Libya, ulimalizika kwa matokeo ya 0-0, kisha nyumbani Simba ikashinda 3-1 na kufuzu makundi. Baada ya kufuzu makundi, Simba imepangwa Kundi A ambapo mchezo wa kwanza imeanzia nyumbani ikishinda 1-0 dhidi ya Bravos ya Angola, huku mchezo ujao ikiwa nchini Algeria dhidi ya CS Constantine.
Msimamo wa Kundi A baada ya mchezo wa kwanza unaonyesha Constantine na Simba zina pointi tatu zote zikishinda mechi za kwanza kwa bao 1-0, huku CS Sfaxien ya Tunisia na Bravos do Maquis hazina pointi.