Eti Cannavaro rais wa ulinzi wa Yanga

Nadir Haroub ‘Cannavaro’
Muktasari:
- Maximo anasifika kwa kutengeneza safu bora za ulinzi ambazo huwa hazipitiki kirahisi katika timu anazofundisha na kwa kuthibtisha hilo, hadi leo Yanga inapoanza mechi za Ligi Kuu Bara haijafungwa hata bao moja huku ikifunga mabao tisa katika mechi tano.
KOCHA wa Yanga, Marcio Maximo mjanja sana, kwani amempa majukumu yote ya safu ya ulinzi nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na beki huyo amekiri kwa kujitapa kuwa yeye ndiye rais wa idara hiyo.
Maximo anasifika kwa kutengeneza safu bora za ulinzi ambazo huwa hazipitiki kirahisi katika timu anazofundisha na kwa kuthibtisha hilo, hadi leo Yanga inapoanza mechi za Ligi Kuu Bara haijafungwa hata bao moja huku ikifunga mabao tisa katika mechi tano.
Safu ya ulinzi ya Yanga inaundwa na Cannavaro na Kelvin Yondani wanaocheza katikati huku pembeni kulia kukiwa na Juma Abdul na kushoto yupo Oscar Joshua na golini akiwepo Deo Munishi ‘Dida’.
Cannavaro aliliambia Mwanaspoti: “Mimi ndiye rais wa ulinzi Yanga, kazi aliyonipa kocha ni kuhakikisha hakipiti kitu mbele ya safu yetu na kama ulivyoona kazi hiyo tunaifanya vizuri kwa kushirikiana na wenzangu.
“Kazi yangu pia ni kuwaelekeza wenzangu pindi mambo yanapoharibika ili tusiruhusu bao kirahisi hapo huwa nashirikiana na Dida ndiyo maana unaona tupo vizuri.”
Ukaribu huu wa Maximo na Cannavaro unatokana na wawili hao kufanya kazi katika kikosi cha Taifa Stars hadi Julai 2010 wakati kocha huyo alipomaliza mkataba wake huku beki huyo akiwa nahodha wake.