Erick Yema, McAthur waanza, Ntibazonkiza akosekana Geita Gold

Mwanza. KIPA mpya wa Geita Gold, Arakaza McAthur raia wa Burundi aliyesajiliwa kutoka Lusaka Dynamos ya Zambia ameanza katika kikosi cha timu hiyo kinachocheza dhidi ya Kagera Sugar muda mfupi ujao saa 10 jioni katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
McAthur alikosekana katika michezo miwili ya kwanza ya timu hiyo ugenini dhidi ya Simba na Azam FC ambayo alidaka Sebusebu Samson ambaye leo ameanzia benchi akiruhusu mabao matano.
Mbali na mrundi huyo, mshambuliaji raia wa DR Congo, Erick Yema ameanza katika safu ya ushambuliaji akisaidiana na nyota waliozoeleka kikosini hapo, Dany Lyanga na George Mpole.
Tofauti na matarajio ya wengi ambao walitazamia kumuona kiungo mshambuliaji, Saido Ntibazonkiza aliyesajiliwa msimu huu lakini mambo yamekuwa tofauti baada ya mchezaji huyo kukosekana kwenye orodha ya wachezaji watakaohusika katika mchezo wa leo licha ya benchi la ufundi kueleza jana kwenye mkutano na waandishi wa habari kuwa atakuwa sehemu ya mchezo.
Tangu alipotangazwa kumalizana na Geita, Saido amecheza mchezo mmoja wa kirafiki wa timu hiyo uliochezwa Jumatano iliyopita dhidi ya Copco Veteran na kuhusika kwenye bao moja katika ushindi wa mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Shule ya msingi Waja mkoani Geita.
Kikosi kamili cha Geita Gold kinachoanza leo ni Arakaza McAthur, George Wawa, Yahya Mbegu, Kelvin Yondani, Bakari Rashid, Kelvin Nashon, Yusuph Kagoma, Edmund John, Daniel Lyanga, George Mpole na Erick Yema
Wachezaji wa akiba ni Sebusebu Samson, Adeyum Salum, Oscar Masai, Ramadhan Chombo, Deusdedith Okoyo, Offen Chikola, Seleman Ibrahim na Jofrey Manyasi.
Geita Gold ilikuwa ya kwanza kufika uwanjani hapo saa 8:40 mchana huku Kagera Sugar ikiwasilia dakika nne baadaye yaani saa 8:44 mchana.