Emery ampiga saluti Pepe

LONDON, ENGLAND. KOCHA wa Arsenal, Unai Emery amemsifu Nicolas Pepe kuwa ni "bonge la mchezaji " wakati klabu yake ikizidi kukabiria kuinasa saini ya winga huyo.
Vyanzo vimethibitisha kwamba Arsenal wanakaribia kukamilisha dili la Euro 80 milioni la kumnasa nyota huo baada ya kuafikiana bei na klabu yake ya Lille wikiendi iliyopita.
Pepe alikuwa akihusishwa na klabu za Liverpool, Manchester United, Napoli na PSG baada ya kufunga magoli 23 na asisti 12 katika michuano yote msimu uliopita, lakini miamba hao wa London kaskazini wameongoza foleni ya kuwania saini hiyo kwa ofay a kulipa mkwanja huo kwa mafungu.
Emery amemwagia sifa winga huyo wa Ivory Coast mwenye umri wa miaka 24, akisema Arsenal itapambana kujiimarisha kabla ya msimu mpya kuanza Agosti 11.
"Klabu inafikiria namna ya kujiimarisha. Kuna wachezaji tofauti mezani," Emery alisema baada ya timu yake kupigwa 2-1 dhidi ya Lyon katika mechi ya kirafiki juzi Jumapili.
"Pepe ni bonge la mchezaji. Tunataka wachezaji ambao hakika wataimarisha kikosi. Tunataka wachezaji bora kwa ajili ya mechi yetu ya kwanza ya msimu ugenini dhidi ya Newcastle."
Aidha, kocha wa Lyon ambaye ni nyota wa zamani wa Arsenal, Sylvinho anaamini Pepe atapata mafanikio Emirates Stadium alipoulizwa anafikiria winga huyo atachezaje England.
“Pepe ni mchezaji wa kiwango cha juu ataiimarisha sana Arsenal," alisema.
Arsenal si klabu pekee iliyoifikia ofa ya Lille kwa winga huyo. Kwa mujibu wa rais wa klabu hiyo, Gerard Lopez, klabu nne zimeafiki kulipa pesa hiyo, akiitaja Napoli kuwa ni mojawapo na akasisitiza ni wakati wa mchezaji mwenyewe kuamua aende wapi.
Pepe, ambaye mkataba wake na Lille unamalizika 2022, amefunga magoli 37 katika mechi 79 tangu ajiunge na klabu hiyo akitokea Angers mwaka 2017.