DTB yabadilishwa jina, kuhamishiwa Singida

UONGOZI wa klabu ya Singida Big Stars zamani DTB umeamua kupeleka makazi ya timu hiyo mkoani Singida huku wakitarajia kuutumia uwanja wa Namfua uliopo mkoani humo kama uwanja wao wa nyumbani.

Wakati klabu hiyo inaitwa DTB, ilikuwa ikiutumia uwanja wa Uhuru uliopo jijini Dar es Salaam kama uwanja wa nyumbani hivyo  baada ya kubadili jina la timu hiyo sasa rasmi itakuwa inatumia uwanja wa Namfua.

Akizungumza na waandishi wa habari Mkurungezi mtendaji wa klabu hiyo, Muhibu Kanu alisema wao kama uongozi wamefanya taratibu zote za kubadili jina la timu hiyo pamoja na kuyaamisha makazi.

"DTB  ilikua inamilikiwa na Benki, sasa timu hii wameichukua wengine na hao wameamua kuibadili jina la timu  na tayari tumeshakamilisha taratibu zote za kisheria" alisema Muhibu na kuongeza;

"Lengo la kuhamia Singida ni kwenda kuwapa fursa wadau pamoja na mashabiki wa soka wa mkoani humo kushuhudia timu yao na kuziona timu zingine za Ligi Kuu."

Mhibu alisema wana kitu cha kujifunza  kupitia timu zilizopanda awali zikitokea chini hivyo na wao wamejipanga vizuri.

"Kupitia timu zilizopanda Ligi kuu msimu uliopita tumejifunza mengi ambayo tumeanza kuyafanyia kazi kwaajili ya kuhakikisha timu yetu inafanya vizuri Ligi kuu Tanzania Bara" alisema Kanu.
 
Pia Mkurungezi huyo alimtambulisha Mkuu wa idara wa habari na mawasiliano wa klabu hiyo ambaye ni Hussen Massanza.