Dodoma Jiji yaizima Coastal Union

Muktasari:
- Huu ni ushindi wa pili mfululizo kwa Dodoma Jiji kufuatia Jumapili iliyopita kuifunga JKT Tanzania mabao 2-1.
Mabao mawili ya Anuary Jabir na Jamal Mtegeta yameipa ushindi Dodoma Jiji leo dhidi ya Coastal Union, mchezo uliochezwa Uwanja wa Jamhuri Dodoma.
Anuary Jabir alifunga bao dakika ya 57 akimalizia pasi nzuri ya Dickson Ambundo, ambapo bao lake ni la pili mfululizo akifunga, akifunga pia mchezo uliopita dhidi ya JKT Tanzania.
Mtegeta akaongeza bao la pili dakika ya 67 kabla ya Coastal kupata bao la kufutia machozi kwa penati iliyopigwa na Raizfin Hafidh dakika ya 83.

Kocha wa Dodoma Jiji, Mbwana Makata amefurahishwa na ushindi huo wa pili mfululizo kwa timu yake na anajipanga kuwakabili maafande Polisi Tanzania mchezo unaofuata.
Matokeo hayo yanaifanya Dodoma Jiji ifikishe alama 28 kwenye msimamo wa ligi kuu, ikipanda na kulingana na KMC katika nafasi ya sita na saba.
Matokeo mengine ya mechi iliyochezwa leo mkoani Morogoro kwenye dimba la Jamhuri ni Mtibwa kulazimishwa sare ya 1-1 dhidi ya Ihefu.
Imeandikwa na Matereka Jalilu