Dk Mwinyi ajitosa ishu ya Zanzibar CAF

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi (kulia) akisaini moja ya jezi zilizozinduliwa juzi kwenye hafla maalumu iliyofanyika visiwani humo.

Muktasari:

  • Kabla ya timu za Zanzibar kuanza kujitegemea kwenye ushiriki wa michuano ya CAF kuanzia 2004, zilikuwa zikiichezea michuano ya kimataifa kupitia Ligi Kuu ya Muungano iliyohusisha timu za Tanzania Bara na Zanzibar na Kombe la Nyerere.  

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imesema bado inapambana ili kupata ufumbuzi juu ya suala la timu ya taifa ya soka ya Zanzibar, 'Zanzibar Heroes' la kutopata nafasi ya kushiriki mashindano mbali mbali yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Hayo yamesemwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi katika hafla ya uzinduzi wa jezi mpya za timu za taifa za Zanzibar, iliyofanyika juzi kwenye Ukumbi wa Nyamanzi, Wilaya ya Magharibi B mjini hapa.

Awali Zanzibar Heroes ilikuwa ikishiriki michuano ya kimataifa ya Kombe la Chalenji inayojumuisha timu za taifa za Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) na kuwahi kushika nafasi ya pili mwaka 2017 zilipofanyika Nairobi, Kenya lakini tangu m,ichuano hiyo isimame kwa timu za wakubwa Heroes imekuwa haina mashindano yoyote inayoshiriki.
Dk Mwinyi amesema anafahamu kuna changamoto kwa Zanzibar Heroes kutopata nafasi ya kushiriki mashindano makubwa yanayoandaliwa na CAF kama vile mashindano ya Mataifa ya Afrika (Afcon) na hata ile ya Chan (inayohusisha timu za taifa za wachezaji wanaocheza katika ligi za ardhi ya Afrika).
"Jezi hizi tunatakiwa tuzitumie katika mashindano ya kuiwakilisha nchi yetu ndani na kimataifa katika madaraja yote na kwa jinsia zote, lakini kumekuwa na changamoto kwa timu kubwa kukosa hiyo nafasi Serikali kwa kushirikiana na Wizara ya Michezo na Shirikisho la Soka (ZFF) tunaendelea kulitafutia ufumbuzi suala hilo na tunayo matumaini makubwa ya kufanikiwa," amesema Dk Mwinyi.

Dk Mwinyi ameongeza,  serikali inaendelea kuimarisha michezo kwa kujenga viwanja vyingine kila Wilaya jambo ambalo litapelekea Zanzibar kuwa na uwezo wa kuwa mwenyeji wa mashindano makubwa ya Kitaifa na Kimataifa kufuatia kuwepo kwa miundombinu ya kisasa.
Amesema serikali inayo azma ya kufundisha makocha ili kuwaongezea umahiri na ujuzi wa michezo mbali mbali, pia inaendelea kuhamasisha uendelezaji na uanzishwaji wa Academy za michezo kwa lengo la kupata wachezaji wazuri watakao iwakilisha nchi katika medani za Kimataifa.
Rais wa klabu ya Yanga, Injinia Hersi Said aliyekuwa mmoja wa wageni waliohudhuria hafla hiyo, amesema uzinduzi huo wa jezi ni jambo kubwa kwa Zanzibar, kwani soka sasa umebadilika tofauti na zamani.

Injinia Hersi amesema jezi hizo zitakwenda kufungua milango ya kibiashara itakayoweza kulinufaisha soka la Zanzibar, ambapo wao Klabu ya Yanga inakusanya  TSH 1.5 Billion kwa mwaka kwenye mauzo ya jezi.
Shirikisho la Soka Afrika (CAF) liliifutia uanachama Zanzibar mwaka 2017 ikiwa ni miezi minne tangu ilipoikubalia kwa madai ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ni mwanachama anayetambuliwa kwa muda mrefu na shirikisho hilo.
Zanzibar ilipewa uanachama huo Machi, mwaka huo wa 2017 kabla ya Julai mwaka huo kuufuta ikikwamisha jitihada zilizokuwa zimefanywa na Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) tangu mwaka 2004 baada ya CAF kufanya mabadiliko ya kuunganisha michuano ya Kombe la CAF na Washindi kuwa Shirikisho Afrika na timu za Zanzibar kukubalika kushiriki kivyao nje ya zile za Tanzania Bara.
Mabadiliko hayo ya kuzitambua timu za Zanzibar kama nchi zilitoa nafasi ya viongozi wa ZFA (sasa ZFF) kupambana kuomba unachama ili visiwani hivyo vitambuliwe kama wanachama nje ya Tanzania ndipo wakapewa uanachama kabla ya kufutwa ndani ya muda mfupi.
Nchi wanachama wa 55 wa CAF waliikubalia Zanzibar bila kufuatwa kwa sheria za shirikisho hilo la Afrika linalozuia uanachama wa mashirikisho mawili kutoka taifa moja na ufafanuzi huo ulitolewa na aliyekuwa Rais wa CAF kipindi hicho, Ahmad Ahmad aliyempokea Issa Hayoutou aliyekuwa ameafiki uanachama huo.