Djokovic ngoma ngumu Australian Open

Djokovic ngoma ngumu Australian Open

TANGU Jumatano wiki iliyopita, staa na bingwa mtetezi wa michuano ya tenisi ya wazi ya Australia (Australian Open), Novak Djokovic amekumbana na vikwazo vya kuingia nchini humo kutokana na msimamo wake wa kutochanjwa chanjo ya Uviko-19.

Mamlaka za nchi hiyo zilizuia kuingia ikiwemo kuzuiwa kwa viza yake, kabla ya timu yake kutumia haki za mahakama kushughulikia suala hilo na kufanikiwa kushinda kesi hiyo, lakini bado haijawa sababu ya kuweza kushiriki michuano hiyo.

Jaji Anthony Kelly ndiye aliyetoa ushindi wa kesi hiyo na kuhoji kipi ambacho staa huyo afanye ili kucheza michuano hiyo, akishangazwa na kitendo cha kuzuiwa kwa viza yake, hivyo akaagiza aachiwe huru na ikibidi acheze michuano hiyo kutetea taji alilobeba mwaka jana.

Hata hivyo, hadi jana Jumanne, suala lake lilitarajiwa kuchukua sura mpya baada ya serikali ya Australia kuwa na nguvu ya kuzuia visa hiyo kupitia mamlaka ya waziri na kama atazuiliwa basi kuna uwezekano mkubwa akafungiwa kuingia nchini humo kwa miaka mitatu.

Kama itakuwa hivyo, inamaanisha Djokovic hatakuwa na nafasi ya kutetea taji hadi 2025.