Diarra, Lomalisa nje Yanga ikiwavaa Coastal Union

Zikiwa zimesalia saa chache kabla ya vinara wa Ligi Kuu Bara Yanga kushuka ugenini kupambana na Coastal Union ya Tanga, imethibitika kuwa mastaa wao wawili kipa Djigui Diarra na beki Lomalisa Mutambala wataukosa mchezo huo.
Yanga itashuka Uwanja wa CCM Mkwakwani kuwania alama tatu mbele ya Coastal Union, mchezo ambao utaanza saa 12:30 jioni.
Yanga imethibitisha itamkosa Diarra ambaye ndio kipa wao namba moja sababu kubwa ikitajwa kuwa majeruhi.
Inaelezwa kipa huyo alilazimika kucheza mchezo uliopita dhidi ya Simba akiwa na maumivu ya bega ambapo madaktari wa timu hiyo wameshauri apumzishwe kwenye mchezo wa Leo.
Yanga bado inaweza kuwa salama licha ya kumkosa Diarra wakiwa na Aboutwalib Mshery anayepewa nafasi ya kwanza ya kuanza huku Metacha Mnata aliyerudishwa kundini akiwa kwenye benchi.
Mbali na Diarra pia Yanga itamkosa Lomalisa ambaye naye anakabiliwa na maumivu na Mkongomani huyo hajasafiri na kikosi hicho kilipotua Tanga juzi usiku.
Kocha wa Yanga Miguel Gamondi bado atakuwa na machaguo mawili ya kuziba nafasi ya staa huyo akiwa na Nickson Kibabage na Kibwana Shomari ambao wanaweza kuchukua nafasi yake.