DC Hanang apongeza bonanza la wanafunzi kuwasaidia kisaikolojia

Hanang. Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Janeth Mayanja amepongeza kufanyika kwa bonanza maalum la michezo kwa wanafunzi kutoka shule nane za msingi walioathirika na maporomoko ya matope wilayani humo na kuwa litawasaidia wanafunzi kisaikolojia na afya ya akili.

Bonanza hilo lililohitimishwa leo Jumapili Januari 21, 2024 katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Katesh, liliandaliwa na Shirika la Save The Children na kushirikisha shule hizo kutoka kata nne zilizoathiriwa na maporomoko hayo yaliyotokea Desemba 3, 2023 na kusababisha vifo vya watu 89 na kujeruhi wengine 139.

Akizungumza wakati wa hitimisho la bonanza hilo, DC huyo amesema kufuatia tukio hilo kila aliyelishuhudia afya yake ya akili haijakaa sawa hivyo kupongeza Shirika hilo ka kukumbuka kundi muhimu la watoto.

“Tunawapongeza wadau wote waliotusaidia katika kipindi cha maafa ikiwemo Save The Children ambao mmekumbuka kundi muhimu la watoto ambalo ni kundi linalobeba kumbukumbu iwe nzuri au mbaya,” amesema na kuongeza

“Kuna baadhi ya watoto wakiona mvua wanaogopa sana, hivyo tunaamini elimu hii ya kisaikolojia mnayoendelea kutoa itasaidia na kuwajenga watoto warudi katika hali zao za kawaida, tunawapongeza sana na tunaomba muangalie na kundi la wanafunzi wa shule za sekondari na vijana chini ya miaka 18,”

Mwakilishi Mkurugenzi wa Shirika hilo, Abdulmajid Faraj amesema lengo la bonanza hilo ni kuboresha afya za akili za watoto ili waweze kuhudhuria masomo na kuwa wataendelea kushirikiana na serikali kuhakikisha watoto na jamii kwa ujumla wanapata kile ambacho ni muhimu baada ya maafa hayo kutokea.

“Toka Desemba 4, 2023 wakati maafa yametokea  tuko hapa kwa nia ya kuishika serikali mkono ili tuweze kuwafikia wale waathirika wa hili tatizo, licha ya misaada ambayo tulitoa, tumeona kutokana na athari zilizojitokeza katika jamii waathriika wakubwa walikuwa ni watoto na hili lilikuwa wazi na limeoneakana baada ya shule kufunguliwa,” amesema Faraj

Ametaja shule zilizoshiriki bonanza hilo lililoanza Januari 11, 2024 kuwa ni Jorodom, Darajani, Kidang’onyi, Bomani, Katesh A, Katesh B, Gendabi na Dumanang ambao wameshiriki michezo ya mpira wa miguu kwa wanafunzi wa kiume na wa kike, kuvuta kamba, mpira kwa wanafunzi wenye ulemavu na mchezo wa kupanga vikombe kwa kutumia maputo (kwa wanafunzi wenye ulemavu).

“Tuliona mahudhurio yalikuwa chini tukaona tutumie huu mwanya kwa kuweka michezo kama chachu ya kuboresha mahudhurio na kwa wakati huo kutumia michezo kama njia bora ya kisaikolojia ya kuponyesha majeraha ya saikolojia na afya ya akili,” ameongeza Faraj

Akizungumza kwa niaba ya shule hizo, Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Jorodom, Balitoga Francis ameshukuru shirika hilo kwa kutoa semina kwa walimu juu ya ulinzi wa mtoto na utoaji wa huduma za kisaikolojia kwa watoto, uanzishaji wa michezo kwa wanafunzi wa shule hizo zilizoathirika na maafa hayo.

“Michezo hii ilikuwa kivutio kwa kuwajenga kisaikolojia na kuwaleta shuleni, mfano Januari 8, 2024 shuleni kwetu wanafunzi walihudhuria asilimia 52 ila Januari 19, 2024 walihudhuria asilimia 98, tunashukuru sana wadau wetu wamesaidia na tunaamini taaluma itakua,”amesema Balitoga

Elizabeth Benedict mwanafunzi wa darasa la saba kutoka Shule ya Msingi Kidang’onyi amesema bonanza hilo limewawezesha kuchangamana na kupunguza maafa yaliyowakumba ambapo baadhi ya wanafuzi wenzao walifariki.

“Kwa kweli michezo imetufurahisha na tunashukuru sana kwa kuwa mmekuja kutusaidia tumesahau yale maafa, nilikuwa nashiriki mchezo wa mpira wa miguu wa wasichana na mashindano yalikuwa mazuri sana na tunaomba wadau michezo hii iendelee,” amesema Elizabeth

Naye Emanuel Samwel kutoka Shule ya Msingi Jorodom amesema michezo hiyo imewapa hamasa na itawasaidia kujijenga kimasomo na kuweza kufanya vizuri.