Dakika 190 za Opah Clement Mexico

Muktasari:
- Opah alijiunga na timu hiyo inayoshiriki Ligi ya Wanawake nchini humo hivi karibuni akitokea Henan Jianye ya China alikocheza msimu mmoja.
DAKIKA 190 alizocheza Mshambuliaji wa Kitanzania, Opah Clement kwenye kikosi cha FC Juarez ya Mexico zimemfanya aendelee kuaminiwa na kocha wa timu hiyo, Oscar Fernandez.
Opah alijiunga na timu hiyo inayoshiriki Ligi ya Wanawake nchini humo hivi karibuni akitokea Henan Jianye ya China alikocheza msimu mmoja.
Tangu atambulishwe kikosini hapo Februari mwaka huu, amekuwa akipata nafasi ya kucheza licha ya kutofunga bao kwenye mechi sita.
Mechi ya kwanza aliyocheza nahodha huyo wa timu ya taifa 'Twiga Stars' ilikuwa Februari 17 dhidi ya chama la rafiki yake, Enekia Lunyamila anayekipiga Mazatlan FC akicheza dakika 19.
Baada ya hapo alikaa benchi mechi mbili mfululuzo kabla ya kucheza dhidi ya Club Tijuana kwa dakika 13, Tigres UANL (1), Atl. San Luis (88), Cruz Azul (51) na Club America (18).
Mtanzania mwenzake Julietha Singano anayekipiga timu moja ameendelea kushikilia nafasi yake akiwa ndiye beki tegemeo katika kikosi hicho.