Coastal Union vs Yanga vita ya pesa

Wakati muda ukizidi kusogea kukaribia pambano la Coastal Union dhidi ya Yanga imeibuka vita mpya ya jeuri ya fedha kuelekea mchezo huo.

Tuanze na wenyeji Coastal Union wao ndani ya dakika 90 wanaweza kujikuta wanaibuka na ushindi na neema kubwa wakiwekewa ahadi ya Sh50 milioni ya kutoka makundi tofauti.

Ofisi ya serikali ya mkoa wao imewaahidi wachezaji wao kiasi cha sh20 milioni endapo wataifunga Yanga kumbuka Mkuu wa Mkoa wa Tanga ni Adam Malima ambaye ni shabiki kindakindaki wa Simba.

Mbali na fedha hizo pia inaelezwa Mbunge wa hapa Ummy Mwalimu ambaye pia ni Waziri wa Afya ametoa ahadi ya sh10 milioni katika ushindi wa timu hiyo.

Inaelezwa pia mdau mwingine ambaye jina lake limefichwa ametoa ahadi ya sh20 milioni endapo wataibuka na ushindi na kufanya jumla ahadi kuwa sh50 milioni.

Mpaka sasa endapo Coastal Union wakipoteza wanauhakika wa kupiga fedha ndefu ya viingilio kutokana na mashabiki watakaofurika uwanjani.

Yanga nao wakajibu mapigo na mezani wamebakiza sh50 milioni tu na wakishinda watakuwa na jumla ya sh70 milioni.

Jana matajiri wa Yanga Frank Kamugisha, Rodgers Gumbo wakiwa na mhandisi Hersi Said waliwakabidhi wachezaji wao sh20 taslimu hata kabla ya wachezaji kuvua viatu walipomaliza mazoezi ya mwisho.

Achana na fedha hizo wamepewa pia ahadi ya sh50 milioni endapo watamaliza kwa ushindi mchezo huo ahadi ikitoka kwa GSM ambao ni wadhamini wao.

Nani atachukua ahadi yake kikamilifu tusubiri matokeo ya firimbi ya mwisho katika Uwanja wa Mkwakwani.