Chomelo: Haukuwa msimu mzuri, tutajipanga

Muktasari:
- Msimu wake wa kwanza 2022/23 alicheza mechi 26 akifunga mabao saba na kutoa asisti 16, huku msimu uliopita 2023/24 akicheza mechi 21 na kufunga manne na asisti tisa.
KIUNGO wa Konya Amputee inayoshiriki Ligi ya Walemavu Uturuki, Ramadhan Chomelo amesema haukuwa msimu mzuri kwa upande wao kutokana na ushindani kuongezeka huku kwa upande wake akitakiwa kufanya majukumu mengi uwanjani.
Akiwa pamoja na Shedrack Hebron anayekipiga Sisli Yeditepe, ni Watanzania pekee wanaosakata soka la walemavu nchini humo ukiwa msimu wa tatu mfululizo sasa na Chomelo aliliambia Mwanaspoti baada ya kumaliza msimu salama, anaamini ujao watajipanga vizuri kwani kwa sasa ligi hiyo inafuatiliwa sana ndiyo maana ushindani umeongezeka.
"Tumemaliza nafasi ya 10 kwenye msimamo, siyo mbaya sana lakini nafikiri hatukuwa vizuri, naamini msimu ujao tutajipanga na kurudi na nguvu," alisema Chomelo na kuongeza;
"Msimu huu sina takwimu nzuri sana kutokana na kufanya majukumu mengi uwanjani kuna muda nabadilishwa kuwa winga, kiungo au hata mshambuliaji."
Msimu huu nyota huyo wa timu ya Taifa ya Tembo Warriors amemaliza msimu akifunga mabao matano na asisti 11.
Msimu wake wa kwanza 2022/23 alicheza mechi 26 akifunga mabao saba na kutoa asisti 16, huku msimu uliopita 2023/24 akicheza mechi 21 na kufunga manne na asisti tisa.