Chirwa aongeza nguvu Azam wakiivaa Kagera Sugar

Muktasari:
Azam katika mchezo uliopita walitoka sare dhidi ya Yanga, huku Kagera Sugar wakifungwa 2-0 na Namungo.
STRAIKA Obrey Chirwa wa Azam Fc, ameongeza nguvu katika kikosi hiko baada ya kuwepo katika msafara wa wachezaji 22 waliosafiri leo asubuhi kwenda mkoani Kagera kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar kesho kwenye Uwanja wa Kaitaba.
Chirwa mwenye magoli nane alikosekana katika timu hiyo tangu walivyorejea kutoka katika mapumziko yaliyotokana na ugonjwa wa COVID-19.
Kocha mkuu wa Azam, Aristica Cioaba amesema amemjumuisha mchezaji huyo katika kikosi chake na atampa muda wa kucheza katika mechi hiyo.
"Ametoka katika majeraha kwa hiyo nitampa muda wa kucheza hata kama sio dakika 90, uwepo wake ni mzuri katika kikosi chetu," alisema.
Kukosekana kwa Chirwa katika mchezo wa Ligi dhidi ya Yanga kulionyesha pengo kubwa baada ya washambuliaji waliocheza kukosa idadi kubwa ya mabao.
Kocha wa Azam, Aristica Cioaba ilimlazimu kumtumia Never Tigere ambaye amezoeleka kucheza kama winga , kucheza kama mshambuliaji wa pili huku akimsimamisha Richard Djodi kama mshambuliaji wa kati huku akizoeleka kucheza kama mshambuliaji wa pili.
Kipindi cha pili aliwaingiza vijana Shaban Chilunda na Andrew Simchimba lakini hawakuweza kuonyesha makeke mbele ya safu ya ulinzi ya Yanga.
Kikosi kilichosafiri,Benedict Haule, Mwadini Ally, Abdul Hamahama, Nicholaus Wadada , Oscar Masai , Abdallah Heri Sebo , Aggrey Moris Lusajo Mwaikenda na Salmin Hoza.
Wengine ni Bruce Kangwa, Idd Nado, Iddi Kipawile, Frank Domayo ,Brayson Raphael,Mudathir Yahya, Never Tigere , Obrey Chirwa,Khlefin Hamdou 'Finito', Richard Djodi, Andrew Simchimba, Shabani Idd Chilunda na Abdallah Masoud Cabaye.