Chippo ataja siri ya Pamba

KOCHA mkuu wa Pamba, Yusuph Chippo amesema siri kubwa ambayo imefanya timu yake ifanye vizuri kwa sasa ni kuhakikisha anaibadilisha kiuchezaji kiujumla na wachezaji wake wamefata falsafa yake.

Chippo ambaye awali alikuwa na timu hiyo inayoshiriki Ligi ya Championship  na baadaye akaenda Ligi Kuu katika klabu ya Coastal Union hakuwa na maelewano mazuri na mabosi wa timu hiyo na kumuondoa lakini tangu arejee Pamba timu hiyo imeanza kuwa tishio.

Akizungumza na Mwanaspoti, Chipo alisema kitu cha kwanza ambacho amekibadilisha ni suala zima la uchezaji wao akiwataka wacheze bila mpira na hata wakiwa na mpira.

"Nimebadili kwanza uchezaji wetu kuanzia eneo la ukabaji, tulitakiwa tuwe tunacheza tukiuwa na mpira au hatuna na hilo limeenda vizuri nashukuru wachezaji wangu kwa kunielewa," alisema Chippo.

Chippo alisema eneo lingine ni kuwatengenezea morali wachezaji wake na kufanyia kazi sehemu la umaliziaji jambo ambalo kwa kiasi kikubwa limekaa sawa hali inayofanya timu ipate matokeo.

"Kampeni yetu kwa sasa ni kuhakikisha timu inapanda daraja kwahiyo nilifanyia kazi eneo la ushambuliaji kuhakikisha tunapata matokeo, tunaendelea vizuri ni jambo jema;

"Tunahitaji matokeo mazuri katika kila mchezo ili tuwe sehemu nzuri kwenye msimamo kwani lengo ni kupanda Ligi."

Pamba inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 41 huku nafasi ya pili ni Kitayosce ikiwa na pointi  42 na upande  wa Ndanda inashika nafasi ya 15 (pili kutoka mwisho) ikiwa na pointi 13.