Prime
Chama na mambo mawili tu Yanga

Muktasari:
- Nyota huyo wa kimataifa kutoka Zambia, inaelezwa kwa sasa anakuna kichwa juu ya mustakabali wake kwa msimu ujao.
KIUNGO mshambuliaji Clatous Chama anayemaliza mkataba na Yanga, ana mambo mawili tu ili kuendelea kuonyesha ukubwa alionao katika soka la Tanzania.
Nyota huyo wa kimataifa kutoka Zambia, inaelezwa kwa sasa anakuna kichwa juu ya mustakabali wake kwa msimu ujao.
Inaelezwa kuwa fundi huyo wa boli ana mambo mawili ya kufanya kwa sasa kuamua aongeze mkataba mpya usiokuwa na dau nono asalie Yanga au aume jongoo kwa meno na kurejesha majeshi Msimbazi iwapo dili linalosukwa kwa sasa litatiki.
Chama, aliyefunga mabao manne na kuasisiti mawili katika Ligi Kuu Bara msimu huu, taarifa za ndani zinasema amekuwa akifanya mazungumzo na kigogo mmoja wa juu wa Simba akiomba kurejea Msimbazi angalau apate muda wa kucheza na kuagana vizuri na mashabiki walioonekana kumkunjia wakati anajiunga na Yanga.
Msimu uliyopita takwimu zake alicheza dakika 1,582, alifunga mabao saba na kuasisti sita kupitia mechi 21, mipira iliyolenga langoni ikiwa ni 17 iliyotoka nje ni 10 na alipomaliza mkataba na Simba alihamia mtaa wa pili ambapo hata hivyo hajaonyesha makali kwa kukosa namba katika kikosi cha kwanza.
Chanzo cha ndani kinasema: “Japo kigogo wa juu Simba kakubaliana na ombi la Chama kurejea, wapo baadhi ya viongozi hawakubaliani nalo wanasema umri wake umekwenda hawaoni kama anaweza akawa msaada kwao kwa muda mrefu, hivyo wanaona wanahitaji kutengeneza vijana wengine wapya zaidi.”
Inaelezwa ukiachana na Simba anayoipigia hesabu, lakini ndani ya Yanga mabosi wanapenda kiungo huyo asalie, lakini kwa kumpa mkataba wa kawaida tofauti na ule waliomng’oa Msimbazi.
“Yanga tayari imeanza mazungumzo na Chama sio kwa presha kama mchezaji ghali kama alivyochukuliwa kutoka Simba msimu uliopita, wanataka kumpa dau la kawaida, hivyo ameachiwa kupima upepo na kutoa uamuzi,” kiliongeza chanzo hicho.
Staa wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Zamoyoni Mogella aliyesema amekuwa akiwashauri wachezaji kabla ya kusaini lazima waangalie nafasi zao katika klabu wanazokwenda kama kuna uwezekano wa kupata nafasi ya kucheza.
“Chama sio mchezaji mbaya alijiunga na Yanga ikiwa na wachezaji katika nafasi yake wakiwa na viwango vya juu Stephane Aziz Ki na Pacome Zouzoua, hii haikuwa rahisi kwake kupenya.”
Mchezaji mwingine wa zamani wa Simba na Yanga, Nurdin Bakari alisema: “Ni kawaida kwa mchezaji anaweza akafanya vizuri timu moja, akienda sehemu nyingine akawa na msimu mbaya, jambo la msingi ni kujitambua na kujua anachokifanya.”
Alisema uwezo wa Chama aliouonyesha Ligi Kuu ni mkubwa hadi msimu wa 2018/19 kuibuka MVP akimaliza na mabao saba na asisti tisa, akisisitiza bado ana nafasi ya kufanya vizuri katika timu kubwa.