Chama la Wana, Geita mzigoni upyaaa

Muktasari:
- Kazi nd’o kwanza imeanza wakati leo Jumamosi ikipigiwa mechi ya mkondo wa kwanza ya mtoano (play-off) kuwania tiketi ya kucheza Ligi Kuu msimu ujao wakati Geita Gold na Stand United (Chama la Wana) zitakapovaana kwenye Uwanja wa Nyankumbu mjini Geita.
KAMA ulidhani mambo yameisha katika Ligi ya Championship baada ya Mtibwa Sugar kubeba ubingwa na kupanda Ligi Kuu Bara sambamba na Mbeya City, pole yako.
Kazi nd’o kwanza imeanza wakati leo Jumamosi ikipigiwa mechi ya mkondo wa kwanza ya mtoano (play-off) kuwania tiketi ya kucheza Ligi Kuu msimu ujao wakati Geita Gold na Stand United (Chama la Wana) zitakapovaana kwenye Uwanja wa Nyankumbu mjini Geita.
Stand United imemaliza nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi ya Championship ikiwa na pointi 61 huku Geita Gold ikimaliza ya nne ikikusanya pointi 56 na kuhitimisha timu mbili za kuchuana play-off ili kuwania kuungana na Mtibwa na Mbeya City zilizochukua nafasi ya KenGold na Kagera Sugar.
Mtibwa Sugar iliyoshuka daraja msimu uliopita, imerejea tena baada ya kuongoza msimamo wa Ligi ya Championship na pointi 71, huku kwa upande wa Mbeya City iliyoporomoka msimu wa 2022-2023, ikirejea kufuatia kumaliza nafasi ya pili na pointi 68.
Stand iliyoshuka daraja msimu wa 2018-2019 katika mechi mbili za msimu huu haijashinda dhidi ya Geita Gold kwani ile ya kwanza ilichapwa ugenini mabao 3-1, Januari 12, 2025, huku marudiano zilipokutana zilitoka sare ya 1-1, Mei 11, 2025.
Timu hizi zinakutana katika mechi ya play-off ambapo mechi ya kwanza inapigwa leo Mei 24, huku ya marudiano ikipigwa Mei 28 na mshindi wa jumla atakutana na atakayepoteza wa Ligi Kuu Bara kwa zitakazomaliza nafasi ya 13 na 14.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Mkuu wa Geita Gold, Mohamed Muya alisema wanatambua mechi itakuwa ni ngumu kutokana na mahitaji ya kila timu, ingawa amewataka wachezaji wa kikosi hicho kutumia vyema uwanja wa nyumbani kabla ya marudiano.
“Tumekuwa na matokeo mazuri mbele ya wapinzani wetu lakini hii ni hatua nyingine ngumu kwa sababu ni ya mtoano na kila mmoja wetu anahitaji kufikia malengo aliyojiwekea, tumejipanga kuhakikisha tunatumia vyema uwanja wetu,” alisema Muya.
Kocha wa Stand United, Juma Masoud alisema mojawapo wa jambo linalompa motisha ni uwepo wa wachezaji wote wa kikosi cha kwanza, ingawa anakwenda katika mechi hiyo kwa tahadhari na kuepuka kazi kubwa ya kufanya watakaporudiana mjini Shinyanga.
“Katika mechi tano zilizopita shida kubwa imekuwa katika eneo la ushambuliaji kwa sababu tumekuwa tunatengeneza nafasi nyingi za kufunga ingawa tulishindwa kuzitumia, tumetumia wiki mbili kurekebisha changamoto hizo zisijirudie,” alisema.
Geita inaingia katika mechi hii ikimtegemea mshambuliaji wa kikosi hicho na kinara wa mabao katika Ligi ya Championship msimu huu, Andrew Simchimba aliyefunga mabao 18, sawa na Raizin Hafidh wa Mtibwa Sugar na Abdulaziz Shahame wa TMA FC.
Kwa upande wa Stand United itaendelea kuwategemea nyota wawili katika eneo la ushambuliaji ambao ni Omary Issa ‘Berbatov’ aliyemaliza msimu akiwa ametupia mabao tisa nyavuni akifuatiwa na mchezaji mwenzake Emmanuel Manyanda mwenye manane.