Chama awatoa hofu mashabiki

Muktasari:

  • Simba itaikaribisha Horoya katika pambano la Kundi C ya michuano hiyo litakalopigwa kuanzia saa 1:00 usiku na ushindi wa aina yoyote utaifanya iungane na Raja Casablanca ya Morocco iliyofuzu mapema ambayo itakuwa ugenini uwanjani pia usiku wa leo kuvaana na Vipers ya Uganda.

KIUNGO fundi wa mpira wa Simba, Clatous Chama amewatoa hofu wanasimba kwa kuwaitwa Kwa Mkapa kwenye pambano la timu hiyo na Horoya AC ya Guinea, huku akiwahakikisha watapata raha kwani wamejipanga kushinda mchezo huo ili kwenda robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba itaikaribisha Horoya katika pambano la Kundi C ya michuano hiyo litakalopigwa kuanzia saa 1:00 usiku na ushindi wa aina yoyote utaifanya iungane na Raja Casablanca ya Morocco iliyofuzu mapema ambayo itakuwa ugenini uwanjani pia usiku wa leo kuvaana na Vipers ya Uganda.

Mastaa wa Simba wakiongozwa na Chama waliwahakikisha mashabiki wa timu hiyo kwamba leo iwe isiwe ni lazima washinde kutokana na walijivyojiandaa na morali waliyonatyo mbali na kuwa uwanja wa nyumbani.

Akizungumza na Mwanaspoti kwa niaba ya wenzake, Chama aliyeshinda tuzo ya Mchezaji Bora wa wiki wa raundi ya nne ya Ligi ya Mabingwa, alisema Simba ina wachezaji bora ambao hadhi yao sio kuishia hatua ya makundi na hilo watalithibitisha leo Kwa Mkapa kwa kuinyoosha Horoya.

"Simba ni timu kubwa, wanachama, mashabiki na wapenzi hawapaswi kuogopa, waje uwanjani na tunawaambia sisi kama wachezaji, hatupaswi kutembea vichwa chini bali kupambana na kuhakikisha tunasonga mbele ili kukutana na wakubwa wenzetu," alisema Chama na kuongeza;

"Sio kama Horoya ni wadogo, ila ukiangalia timu yetu ina wachezaji wengi wazoefu na bora ambao wanaijua vyema michuano hii, mechi itakuwa ngumu lakini naamini tutashinda na kusonga mbele."
Chama anayesifika kwa kutengeneza nafasi zaidi aliongeza kwa kusema ndoto ya kila mchezaji anayecheza Afrika ni kufika mbali kwenye Ligi ya Mabingwa na mastaa wote wa Simba kwa sasa wanawaza kufanya vizuri huko ili kujenga wasifu wao na kuipa heshima klabu.

"Kila mchezaji wa ndani moja ya malengo yake ni kucheza Ligi ya Mabingwa na kufanya vizuri kwani hii ndio michuano mikubwa barani Afrika. Kwetu Simba kila mmoja anataka kufanya vizuri huko, ari ya upambanaji ipo juu kwani tukifanya vizuri huku ni faida kwetu na kwa klabu kwa ujumla hivyo mashabiki waje kwa wingi kutusapoti, tutawafurahisha," alisema Chama.

Simba iko nafasi ya pili kundini C ikiwa na pointi sita nyuma ya Raja yenye pointi 12 huku Horoya ikiwa nafasi ya tatu na pointi nne na Vipers ikiburuza mkia na pointi moja baada ya mechi nne.