Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

CAF yapasua ukuta Yanga

Muktasari:

Kikosi cha Yanga kina jumla ya mabeki nane, kati ya hao wa wanne ni mabeki wa kati ambao ni nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani, Mbuyu Twite, Vicent Bossou na Patrick Ngonyani, huku wale wa pembeni ni Juma Abdul, Haji Mwinyi Mngwali na Oscar Joshua.

YANGA hailali, ikipiga hesabu zake itoke vipi katika Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo itashiriki mwakani, lakini huku nyuma wadau wawili wa soka wamepata wasiwasi juu ya safu ya ulinzi ya timu hiyo hasa baada ya kipigo cha mabao 7-0 ilichopewa Taifa Stars na timu ya Algeria.

Stars ilikandikwa mabao hayo katika pambano la marudiano la kuwania tiketi ya kucheza makundi ya kusaka kwenda Fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2018 zitakazofanyika Urusi, huku asilimia kubwa ya ukuta wa kikosi hicho cha Tanzania kikiundwa na wachezaji wa Yanga.

Katika michuano ya kimataifa ya Caf, mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Bara, mwaka huu ilikwamia raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Etoile du Sahel ya Tunisia iliyofika fainali.

Kikosi cha Yanga kina jumla ya mabeki nane, kati ya hao wa wanne ni mabeki wa kati ambao ni nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani, Mbuyu Twite, Vicent Bossou na Patrick Ngonyani, huku wale wa pembeni ni Juma Abdul, Haji Mwinyi Mngwali na Oscar Joshua.

Akizungumza na Mwanaspoti mchambuzi wa soka nchini na nyota wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Ally Mayay, alisema Yanga inaundwa na wachezaji wengi wazoefu, ila bado tatizo kubwa ni kwamba mabeki wengi wamekuwa wakishindwa kufanya vyema katika mechi za kimataifa.

“Ubora wa baadhi ya wachezaji wetu ni mzuri kwa kuwa hapa ndani wanakabana na mastraika wengi ambao wanatabirika lakini tukitoka nje hali inakuwa mbaya hilo ni tatizo la ubora na halipo Yanga pekee hata Azam pia wanalo kwa kiasi fulani,” alisema Mayay.

Kocha mkongwe na msomi Mshindo amelitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na benchi la ufundi la timu ya taifa kutambua kuwa nyota wa Yanga na Azam wanaocheza katika timu ya taifa nao ni binadamu hivyo wapewe mapumziko kuliko kuwatumia mfululizo kama ilivyo kwa sasa.

“Hawa wachezaji nao ni binadamu, wanatakiwa kupumzishwa, wamecheza mfululizo sana na hawajapumzika, wanaweza kuzigharimu timu zao kwa kushindwa kucheza vizuri katika mechi za mzunguko wa pili.

“Sikuona kama kulikuwa na ulazima wa kwenda nao katika Kombe la Chalenji, tungechukua wachezaji wapya ili hawa wapumzike, hii ingetusaidia zaidi kuliko tunavyofanya sasa kuwatumia wachezaji wale wale, huku ni kuwachosha zaidi,” alisema Msolla.

Hali ilivyo

Katika hali ilivyo sasa, Yanga ina jumla ya mabeki watatu ambao wapo katika vikosi vya Zanzibar Heroes na Kilimanjaro Stars kabla ya kutawanyika huko wakiwa na Taifa Stars.

Mabeki hao wamekuwa wakishindwa kufanya vyema hali ambayo ni wazi itashusha hali ya kujiamini kumbukumbu mbaya ikiwa ni kukubali kipigo cha mabao 7-0 dhidi ya Algeria ambapo katika mchezo mabeki wa Yanga wakiwa Cannavaro, Yondani, Mwinyi na kipa Ally Mustapha Barthez.

Hata kama timu hucheza kitimu, lakini kipigo hicho cha Algeria ni kama kimewaathiri zaidi mabeki wa Yanga kuelekea michuano hiyo ya Caf mwakani ambapo ratiba yake inatarajiwa kutolewa hivi karibuni.

Kauli ya uongozi

Akizungumzia hilo, Katibu Mkuu wa Yanga Dk Jonas Tiboroha amesema kwao hoja hiyo wanaiangalia katika mitazamo miwili tofauti ambapo kwanza ametamka kwamba kikosi chao licha ya kwamba Cannavaro na Yondani kuwa ndiyo wanaocheza sana bado wana chaguo la kutosha endapo watapata wasiwasi juu ya mabeki hao wakongwe nchini.

“Unajua ukiangalia ni kweli kwa namna fulani ni kweli kuna haja ya wenzetu kuangalia uwezekano wa kuwapumzisha hawa wachezaji wetu wengi wao wamecheza sana kuna mechi ambazo hazina umuhimu kwao kucheza wangepewa nafasi hizo wachezaji wachanga, hawa wakongwe wacheze kulingana na umuhimu wa mechi husika,” alisema Tiboroha.

Hata hivyo Katibu huyo akaweka bayana kwamba hawana maamuzi kwani jukumu la uchaguzi wa wachezaji ni kazi ya kocha.

“Jukumu la kuchagua mchezaji ni la kocha sisi Yanga tunasubiri kocha atuambie anahitaji nini hata  akitaka tumsajilie beki mwingine tutaangalia, lakini ni kweli kwamba tunahitaji kuwa na safu thabiti ya ulinzi.

Kocha Pluijm

Kocha Mkuu wa Yanga, Hans Van Pluijm alikiri kuwa matokeo ya dhahama iliyoyapata Stars kutoka kwa Algeria imewaondolea mabeki wake, Yondani, Cannavaro na Mwinyi hali ya kujiamini.

Pluijm alisema kitendo cha nyota hao kucheza dhidi ya nyota wakali duniani kama Yacine Brahim wa FC Porto, Islam Sliman wa Sporting Lisbon na Riyard Mahrez wa Leicester City kingeweza kuwa na matokeo chanya kwao kama wangefanya vizuri lakini kipigo walichopata kimewaharibu kabisa.

“Wangefanya vizuri ingekuwa ni msaada kwetu katika michuano ya kimataifa mwakani lakini bahati mbaya imekuwa tofauti, mabao 7-0 ni mengi sana kusema kuwa imewasaidia,” alisema Pluijm.

“Kama watafanya vizuri katika michuano ya Chalenji wanaweza kurejesha hali yao ya kujiamini, lakini hii michuano ubora wake bado uko chini sana, haiwezi kutusaidia sana,” alifafanua kocha huyo Mdachi.