Bwalya aagwa kibabe Simba

Sunday June 19 2022
FULL PIC
By Ramadhan Elias

SIKU ya leo itabaki kuwa kumbukumbu kwa kiungo wa Simba Rally Bwalya baada ya kuagwa rasmi kwa Wekundu wa Msimbazi hao huku akisindikizwa na ushindi wa mabao 3-1.

Ilikuwa kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya KMC uliopigwa kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa na nje ya kuwa mechi ya ligi lakini Simba imeitumia kumuaga kiungo wake huyo iliyemuuza Amazulu FC ya Afrika Kusini.

Bwalya alijiunga na Simba mwanzoni mwa msimu uliopita akitokea Power Dynamos ya Zambia na katika kipindi alichokaa kikosini hapo amekuwa  akicheza eneo la kiungo na kuisaidi kushinda makombe ikiwemo la Ligi Kuu msimu uliopita.

Katika mchezo huo, timu zote zilianza kucheza kwa utulivu huku pasi fupi fupi zikipigwa kwa pande zote mbili.

Kipindi cha kwanza kilimalizika Simba ikiwa nyuma kwa bao 1-0, lililofungwa na winga wa KMC, Hassan Kabunda dakika ya 41.

Kipindi cha pili kilirejea kwa Simba kufanya mabadiliko kwa kumtoa kiungo mkabaji Sadio Kanoute na kuingia  mshambuliaji Peter Banda.

Advertisement

Ingizo la Banda lilionekana kuzaa matunda na kuifanya Simba kuongeza kasi ya mashambulizi langoni kwa KMC.

Dakika ya 51 Simba ilipata bao la kusawazisha lililofungwa na Kibu Denis akimalizia krosi ya Pape Sakho.

Baada ya bao hilo, KMC ilifanya mabadiliko ya wachezaji wawili kwa kuingia Kenny Ally na Abdul Hilaly waliochukua nafasi za Awesu Awesu na Miraji Athuman.

Hata hivyo mabadiliko hayo hayakuisaidia KMC kwani dakika ya 62 Simba ilipata bao la uongozi likifungwa na Sakho.

Dakika tatu baadae Simba ilipata bao la tatu kupitia kwa Henoc Inonga akifunga kwa kichwa mpira wa krosi uliopigwa na Sakho.

Baada ya bao hilo Simba iliendelea kutafuta bao la nne lakini umakini kwenye eneo la mwisho ulipungua na matokeo kusalia hivyo hadi dakika ya 90.

Kibu,  Sakho na Erasto Nyoni walifanyiwa mabadiliko na nafasi zao kuchukuliwa na Meddie Kagere, Taddeo Lwanga na Jimmyson Mwanuke.

Dakika ya 86, Simba ilimtoa Bwalya na kuingia Yusuph Mhilu ambaye hakubadili matokeo na mechi kumalizika kwa Simba kushinda 3-1.

Ushindi huo unaifanya Simba kufikisha alama 57 katika nafasi ya pili kwenye msimamo huku KMC ikibaki na pointi zake 32 nafasi ya 10.

Advertisement