Bundi atua KMC

KMC inakabiliwa na  majeruhi sita ya wachezaji wake wa kikosi cha kwanza ambao kila mmoja jambo linaloipa wakati mgumu timu hiyo.

Kabla ya mechi ya jana ugenini dhidi ya Singida Big Stars, Watoza ushuru hao wa Kinondoni walikuwa na wachezaji majeruhi watatu ambao ni beki wa pembeni Kelvin Kijiri na viungo Ally Awesu na Emmanuel Mvuyekure lakini hadi dakika 90 za mchezo huo zinamalizika walikuwa wameongezeka watatu na kufika sita.

Wachezaji walioumia jana wakati KMC ikipoteza kwa kuchapwa 1-0 ugenini na Singida ni beki Hance Masoud aliyekimbizwa Hospitari na gari ya wagonjwa katika kipindi cha kwanza na wengine ni Kiungo Baraka Majogoro na beki Ibrahim Ame walioumia na kushindwa kuendelea na mchezo.

Ofisa habari wa timu hiyo, Christina Mwagala amethibitisha hilo na kueleza mipango yao; "Kwasasa tunakabiliwa na changamoto kubwa ya wachezaji wenye majeraha, na ukiangalia kwenye timu kila mchezaji ana mchango mkubwa pindi anapopewa majukumu na kocha, hivyo ni kipindi kigumu lakini tutajitahidi kadiri tuwesavyo ili kufanya vizuri kwenye michezo inayokuja," alisema Mwagala na kuongeza;

"Katika hatua nyingine KMC FC imerejea Jijini Dar es salaam alfajiri ya leo ikitokea mkoani Singida na kesho itaanza kufanya maandalizi ya mchezo unaokuja dhidi ya Tanzania Prisons utakaopigwa Novemba 28 katika uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam."

KMC inayonolewa na kocha Mnyarwanda Thierry Hitimana haijashinda mechi tano za mwisho ilizocheza ikiambulia sare moja tu na kupoteza nne na ipo nafasi ya 10 kwenye msimamo na alama 14 ilizovuna kwenye michezo 13.