Bocco aichungulia Polisi Tanzania

WAKATI mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Polisi Tanzania FC dhidi ya Simba SC ambao utapigwa leo Jumapili kwenye uwanja wa Ushirika Moshi ukisubiriwa kwa hamu kubwa mshambuliaji wa Simba John Bocco ndiye kinara wa ufungaji timu hizo zinapokutana.

Timu hizo zimekutana mara Sita katika michezo ya Ligi Kuu huku Simba ikishinda mara tano na kutoka sare mchezo mmoja wakati Bocco yeye akiwa ndiye kinara wa ufungaji baada kuweka kambani mabao matatu.

Alianza kufunga mara ya kwanza timu hizo zilipokutana msimu wa 2019/20 ilikuwa ni February 4-2020 ambapo Simba ilishinda mabao 2-1, mchezo uliopigwa uwanja wa Taifa Dar.

Katika mchezo huo Bocco aliisawazishia Simba dakika ya 57 baada ya kutanguliwa na Polisi Tanzania kwa bao la mapema dakika ya 22 kupitia kwa Sixtus Sabilo ambaye kwa sasa anakipiga Mbeya City FC kisha Ibrahim Ajibu akaifungia Simba bao la pili na la ushindi.

Bocco alifunga tena mabao mawili katika mchezo wa mwisho wa msimu huo ambao ulipigwa Julai 26 katika uwanja wa Ushirika Moshi, Simba ikishinda 2-1, akifunga dakika ya 2 na 45 huku bao la Polisi likifungwa na Marcel Kaheza dakika ya 30.

Kwa sasa ni kama amerejesha tena makali yake baada ya kufunga mabao matatu (hat trick), kwenye mchezo dhidi ya Ruvu Shooting ambao Simba ilishinda mabao 4-0 na kuwa mchezaji wa pili kufungahat-trick Ligi Kuu baada ya Fiston Mayele wa Yanga kufanya hivyo dhidi ya Singida Big Stars.

Wengi wanasubiri kuona kama naodha huyo mwenye mafanikio makubwa ndani ya Simba SC ikiwemo kuifikisha timu robo fainali ya Klabu Bingwa Afrika mara mbili na robo fainali Kombe la Shirikisho mara Moja lakini pia ubingwa mara nne wa Ligi Kuu Bara kama ataendeleza ubabe tena dhidi ya Polisi Tanzania leo.