Bocco aanza kuivutia kasi Prisons

Muktasari:

Bocco amepachika bao moja katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu ambalo lilikuwa ni dhidi ya Ihefu katika mechi ya kwanza ya ligi ambayo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Baada ya kukosekana katika mechi tatu mfululizo zilizopita za Ligi Kuu, nahodha wa Simba, John Bocco huenda atarejea uwanjani katika mchezo unaofuata wa Simba dhidi ya Prisons mkoani Rukwa, Oktoba 22

Mshambuliaji huyo licha ya kuanza vyema msimu huu kwa kuichezea Simba, mechi mbili za mwanzo dhidi ya Ihefu na Mtibwa ambazo alifunga bao moja, alishindwa kuonekana katika mechi zilizofuata dhidi ya Biashara United, Gwambina na JKT Tanzania kutokana na majeraha.

Hata hivyo nyota huyo bila shaka sasa anarudisha matumaini katika kikosi hicho baada ya leo kuanza mazoezi ambayo pia ni maandalizi kwa ajili ya mechi dhidi ya Prisons.

Katika mazoezi hayo ambayo yanafanyika kwenye Uwanja wa Mo Simba Arena uliopo Bungu, Bocco ameonekana kupewa programu ya peke yake ambapo wakati wenzake wakifanya mazoezi ya viungo na kisha baadaye yale ya ufundi na mbinu, yeye ametakiwa kuzunguka uwanja huo kwa kutembea akiwa anasimamiwa na mtaalam wa viungo, Adel Zrane na daktari wa timu, Yassin Gembe.

Mwanzoni wakati Bocco akifanya mazoezi hayo ya kutembea, wachezaji watano ambao waliitwa katika timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', Mzamiru Yassin, Mohamed Hussein, Said Ndemla, Jonas Mkude na Shomari Kapombe walikuwa wakifanya mazoezi ya kukimbia ingawa baadaye walikwenda kujiunga na wengine katika mazoezi ya mbinu na ufundi.

Katika mechi mbili ambazo Bocco alicheza, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ihefu ambao alifunga moja na mwingine dhidi ya Mtibwa walitoka sare ya bao 1-1.