Boban, Redondo wana jambo lao Arusha

Muktasari:
- Nyota hao na wale wa klabu za nchi za Kenya, Uganda na Rwanda wanatarajiwa kuchuana katika michuano maalumu inayowahusisha wachezaji wa zamani (Cecafa Veterans) inayoanza kesho Ijumaa kwenye Viwanja vya TGT, kilichopo Kisongo jijini humo.
NYOTA mbalimbali waliowahi kucheza kwa mafanikio makubwa katika michuano ya Kombe la Klabu za Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) wakiwamo Haruna Moshi 'Boban', Abdallah Kibadeni, Ramadhani Chombo 'Redondo' na wengine wana jambo lao jijini Arusha kuanzia kesho Ijumaa.
Nyota hao na wale wa klabu za nchi za Kenya, Uganda na Rwanda wanatarajiwa kuchuana katika michuano maalumu inayowahusisha wachezaji wa zamani (Cecafa Veterans) inayoanza kesho Ijumaa kwenye Viwanja vya TGT, kilichopo Kisongo jijini humo.
Mashindano hayo yatafanyika kwa siku mbili kesho Ijumaa na Jumamosi ikishirikisha timu kutoka ncghi sita ikiwamo wenyeji Tanzania na Benin, mbali na Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.
Kila nchi itawakilishwa na timu moja isipokuwa Tanzania ambayo imeingiza timu mbili ambazo ni Arusha All Stars Veterans na Gymkhana Veterans kutoka Dar Es Salaam.
Pia kwa mara ya kwanza katika historia ya mashindano ya Cecafa Wazee imeshuudiwa timu kutoka nje ya Afrika Mashariki na Kati ambayo ni Benin inayoshiriki kama mgeni mwalikwa kupitia timu ya Wizara ya Fedha ya nchi hiyo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Cecafa Wazee 2025, Francis Oiro amesema maandalizi yamekamilika tayari droo imepagwa kila kundi itakuwa na timu tatu na zitacheza kwa dakika 90 ambapo washindi wawili wa juu watatinga nusu fainali.
"Mashindano ya mwaka huu pia yana utofauti kwani mbali na Cecafa ya Wazee pia kutakuwa na Cecafa ndogo ambayo hii itajumuisha wale wachezaji ambao watakosa usajili kwenye mashindano rasmi," alisema Oiro na kuongeza;
"Usajili kila timu mwisho ni wachezaji 25 na unakuta timu moja ina wachezaji 50 hivyo tumeona ni vyema pia wale wengine tuwawekee mashindano yao."
Ameongeza mashindano ya Cecafa Wazee yanalenga kuitangaza Utalii wa nchi kupitia michezo' lakini pia kuwakutanisha pamoja wachezaji wa zamani ambapo kama wanadaaji wanatarajia yatakuwa na upekee kuanzia kwenye mpangilio wa uendeshaji lakini pia burudani ambazo zitakuwepo nje na ndani ya uwanja.
"Baada ya mashindano kuisha kuna timu zitapata nafasi ya kutembelea hifadhi zetu na kufanya Utalii mfano Benin wataenda Zanzibar pia Bunge la Kenya wataenda kutalii Ngorongoro," amesema Oiro.
Oiro alisema Nyota mbalimbali ambao wametamba na timu mbalimbali za Afrika Mashariki zikiwemo Yanga,Simba,APR,URA,SC Villa "Jogoo",Gor Mahi ,AFC Leopards,Rayon Sports,Tusker na zingine nyingi watakuwepo wakionyesha ufundi wao na kutoa burudani kwa wapenzi wa soka Arusha.
"Sunday Manara 'Computer', Abdallah Kibadeni 'King Kibadeni', Haruna Moshi 'Boban', Ramadhan Chombo 'Redondo', Philipo Alando, Aziz Nyoni ni miongoni mwa mastaa ambao watakuwepo," amesema Oiro.
Denis Shemtoi ni Katibu Mkuu wa Arusha All Stars ambao ndio wenyeji anasema maandalizi yao yapo vizuri kila kitu kiko sawa ndani na nje ya uwanja hivyo mashabiki wajitokeze tu kushuudia burudani.
"Tumefanya usajili kadhaa kuelekea michuano hii kuongeza nguvu katika kikosi chetu ili tufanye vizuri kuna wachezaji wakubwa sana mtawaona leo," amesema Shemtoi.
Rashid Idd 'Chama', nyota wa zamani wa kimataifa wa Yanga na timu ya taifa, Taifa Stars pia kocha wa zamani wa timu ya Mashujaa FC ya Kigoma ambaye kwa sasa ni kocha wa Arusha All Stars alisema sehemu ambazo zilikuwa na mapungufu ambayo ni safu ya ushambuliaji na Ulinzi amefanyia kazi hivyo kila kitu kiko sawa kwenye kikosi.
Cecafa ndogo itashirikisha timu za Bunge la Kenya, Railways za Kenya, Sea Club ya Uganda, Chuo Kikuu cha Nelson Mandela, Revolution, NMB zote kutoka Arusha".
Cecafa kubwa ambayo ndio mashindano kamili kutakuwa na timu ya Wizara ya Fedha ya Benin, Kenya Railways, Ghymkhana, Arusha All Stars za Tanzania, Sea Club ya Uganda na Africa Veterans kutoka Rwanda.