Biko Scanda anukia CEO mpya Pamba

Muktasari:

  • Taarifa kutoka ndani ya kikosi hicho zimeiambia Mwanaspoti kwamba, vikao vya ndani vinaendelea kwa ajili ya kumpata mtendaji mkuu baada ya mkutano uliofanyika Juni, mwaka huu jijini Mwanza kushindwa kupata mtu sahihi.

KLABU ya Pamba Jiji iko katika mazungumzo na Biko Scanda ili awe mtendaji mkuu mpya kwa ajili ya msimu ujao.

Taarifa kutoka ndani ya kikosi hicho zimeiambia Mwanaspoti kwamba, vikao vya ndani vinaendelea kwa ajili ya kumpata mtendaji mkuu baada ya mkutano uliofanyika Juni, mwaka huu jijini Mwanza kushindwa kupata mtu sahihi.

"Mazungumzo baina ya klabu na yeye yanaendelea vizuri na kila kitu kitakapokamilika tutakiweka wazi ila itoshe kusema ni kweli na kwa sasa yupo Mwanza. Tuna imani kubwa na uwezo wake hivyo acha tuone kitakachoamuliwa," kimesema chanzo kutoka ndani ya Pamba Jiji.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mwenyekiti wa Pamba, Bhiku Kotecha amesema kama ambavyo wamekuwa wanatoa taarifa za klabu kwenye mitandao ya kijamii wataendelea kufanya hivyo, huku akiwaomba mashabiki watarajie mambo makubwa.

"Kwa sasa akili zetu kubwa ni kutengeneza kikosi bora kitakacholeta ushindani msimu ujao, ndio maana hata wachezaji wote ambao tumewasajili unaona wana ubora mkubwa. Suala la nafasi ya mtendaji mkuu muda ukifika tutaliweka wazi," amesema.

Itakumbukwa kabla ya timu hiyo kupanda Ligi Kuu Bara ilikuwa inaongozwa na Ofisa Mtendaji Mkuu, Alhaji Majogoro ambaye amebadilishiwa majukumu baada ya mkutano mkuu kumuondoa na kumteua ili awe mjumbe wa bodi.

Endapo Biko atapewa nafasi hiyo itakuwa ni mara ya pili kuongoza akiwa mtendaji mkuu wa klabu baada ya Novemba 22, mwaka jana kuteuliwa Ihefu (sasa Singida Black Stars) na kudumu siku 44 ambapo aliondolewa Januari 4, mwaka huu.