Prime
Cape Verde na mkakati nadhifu wa dispora
Muktasari:
- Kwa ilionekana kama Cape Verde ilibahatisha kutoka sare ya bila kufungana na Hispania iliyosheheni wachezaji wenye vipaji na iliyopiga mashuti 25. Ushujaa wa kipa mwenye umri wa miaka 40, Vozinha na nidhamu ya kujilinda ya timu nzma ulizuia nyota kama Yamal kuziona nyavu.
Gumzo kubwa kwa sasa barani Afrika ni mwenendo wa taifa la Cape Verde kwenye fainali za Kombe la Dunia baada ya timu hiyo kuonyesha nidhamu ya hali ya juu ya kimchezo ilip[okutana na mabingwa wa Ulaya, Hispania na kutoka naos are ya bila kufungana kabla ya kulazimisha sare nyingine ya mabao 2-2 na mabingwa wa zamani wa dunia Uruguay.
Kwa ilionekana kama Cape Verde ilibahatisha kutoka sare ya bila kufungana na Hispania iliyosheheni wachezaji wenye vipaji na iliyopiga mashuti 25. Ushujaa wa kipa mwenye umri wa miaka 40, Vozinha na nidhamu ya kujilinda ya timu nzma ulizuia nyota kama Yamal kuziona nyavu.
Hata hivyo, sare nyingine ya mabao 2-2 na Uruguay ilidhihirisha kuwa Cape Verde si timu ya kuidharau na sasa inanusa hatua ya 32 bora, ikiwa inashiriki fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza.
Wengi wanaweza kuwa wamestushwa na mafanikio hayo, lakini wanaoifuatilia Cape Verde au Nyangumi wa Bluu watakuwa walishaona dalili njema baada ya taifa hilo dogo kuongoza kundi la kufuzu kwa fainali hizo lililokuwa na nchi za Cameroon, Angola, Libya, Mauritius na Eswatini.
Michuano hiyo ilionyesha kuwa Cape Verde ilikuwa na uwezo wa kushinda mechi ngumu, kustahimili ukali wa timu pinzani na kuwa na mwendelezo wa aina ya uchezaji.
Taifa hilo lenye watu 525,000 halina muda mrefu tangu lianze kushiriki mashindano ya kimataifa. Lilijiunga na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) mwaka 1978 na baadaye Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) mwaka 1982.
Tangu wakati huo limeshashiriki fainali za Mataifa ya Afrika mara nne (2013, 2015, 2021 na 2023), likifika hatua ya robo fainali mwaka 2013 na 2023.
Hakuna shaka kuwa mafanikio ya Cape Verde yanatokana na taifa hilo kutumia zaidi wachezaji waliokuzwa na kukulia barani Ulaya, lakini hiyo si sababu pekee. Ni uamuzi na mkakati wa muda mrefu uliowekwa na viongozi wa Shirikisho la Soka la Cape Verde (CVFF) tangu mwishoni mwa mwaka 2000.
Uamuzi ulikuwa ni kutumia hazina waliyonayo ya vijana wengi wenye asili ya Cape Verde walio barani Ulaya. Wengi wako katika nchi kama Ureno, Ufaransa, Uholanzi na Luxembourg. Vijana wengi wa Cape Verde huhamia Ureno, nchi ambayo ni mwendo wa chini ya saa moja.
“Tumekuwa tukijenga mradi huu hatua kwa hatua. Hakuna kitu kinachoweza kutokea usiku mmoja. Wachezaji wanaelewa utambulisho wa timu na kila mmoja anafanya kazi kufanikisha lengo moja,” alisema kocha wa Cape Verde, Pedro Bibista Brito akikaririwa na New Times la Rwanda.
“Watu wanaiona Cape Verde sasa kwa sababu ya Kombe la Dunia, lakini safari hii ilianza miaka mingi iliyopita. Tumejitahidi kutengeneza heshima. Tumeonyesha kuwa tunaweza kushindana dhidi ya timu bofra duniani.”
Tofauti na mataifa makubwa katika soka, Cape Verde haina mchezaji ambaye ni nyota au mkubwa kuliko wengine badala yake imejenga timu katika misingi ya nidhamu ya mchezo, umoja na imani kuwa inaweza.
Kwa hiyo, Cape Verde imeonyesha kuwa mafanikio hayawezi kuja kwa sababu tu nchi ina wachezaji wengi waliokulia au kukuzwa barani Ulaya, au ina ni taifa la soka, au ina fedha, bali ni mikakati imara, utafutaji nadhifu wa vipaji na mwendelezo wa mikakati na mbinu badala ya kubadilishabadilisha mipango.
Nchi nyingi zina wachezaji wenye asili ya Afrika waliokulia barani Ulaya, lakini hazijawa na mikakati sahihi ya kuwatumia. Wakati mwingine timu za Afrika hujikuta kwenye migogoro na wachezaji kwa kushindwa kuwalipa posho zao kwa Imani kuwa ni matajiri kwa kuwa wanalipwa mishahara mikubwa kwenye klabu zao.
Wachezaji kama wa Cameroon hugoma si kwa sababu hasa ya kutolipwa posho hizo, bali kutaka kuonyesha kuwa ni muhimu kukawa na utawala bora. Yaani kama unamnyima mchezaji wa taifa posho yake, kiongozi husika anaweza kuelekeza fedha za shirikisho katika mipango ya maendeleo?
Mkakati wa kutumia wachezaji waliokulia nje ni lazima uwe makini katika kuishi nao, katika kuwateua na katika kuhakikisha soka la ndani linaendana na kasi ya maendeleo. Zaidi ya yote, kujua kama nchi ina hazina ya wachezaji wenye asili yake nje.
“Kuichezea Cape Verde ni kuwakilisha miziz yetu na familia zetu,” anasema Ryan Mendes, nahodha wa muda mrefu wa Cape Verde.
“Wengi wetu wamekulia nje lakini wakati wote tunajisikia kuunganishwa nan chi yetu. Kuvaa jeszi hii kunabeba ndoto za gtaifa zima.”
Nchi za barani Ulaya na Marekani hunufaika na wageni wanaozaliwa au kukulia huko au wenye uchotara kutokana na ukweli kuwa chaguo la kwanza la mchezaji chotara ni kuchezea nchi hizo.
Niliongea na Kelvin-Prince Boateng jijini Berlin, Ujerumani kabla ya fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2006 kuhusu uwezekano wa kuichezea Ghana baada ya kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia. Mchezaji huyo ambaye ana uraia pacha, alisema hangekubali wito wa kuchezea taifa hilo la Afrika kwa sababu halikushiriki kwa namna yoyote kumkuza.
Alikuwa na matarajio ya kuitwa timu ya taifa ya Ujerumani, lakini ni kaka yake aliyeteuliwa. Alipoona amekosa nafasi Ujerumani ndipo alipoamua kuichezea Ghana.
Kwa hiyo, wengi wanaokubali kuchezea mataifa ya Afrika ni wale ambao hawana nafasi ya kuchezea nchi za barani Ulaya.
Ni kutokana na hilo, Cape Verde ilitengeneza mkakati nadhifu wa kuteua wachezaji ambao watakubaliana na nidhamu waliyoiweka na wale wenye nia hasa ya kulitumikia taifa hilo badala ya kutafuta wachezaji nyota ambapo huweka kiburi mbele.
Pia, hata kama tuna hazina kubwa ya wachezaji nje ya nchi, hatuna budi kuwa na mikakati imara ya kuendeleza soka ndani. Wachezaji wengi huuliza maswali mengi kabla ya kukubali wito na zaidi huvutiwa na mwenendo wa timu ya nchi inayowataka na ndio huwa kichocheo.
Kutegemea wachezaji waliokulia nje pekee ni njia ya mkato ambayo haiwezi kujenga soka la ndani na ambayo mafanikio yake si ya kudumu.